Serikali imesema itawajengea uwezo makandarasi wadogo wanaotumia teknolojia ya nguvukazi (Labor Based Technology) katika ujenzi na ukarabati  wa matengenezo ya barabara, madaraja na majengo ili kuhakikisha kuwa wanapata fursa zaidi za kushiriki na kushindana katika kazi zilizotengwa mahsusi kwa ajili makandarasi hao.

Hayo yalibainishwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano anayeshughulikia Sekta ya Ujenzi, Arch. Elius Mwakalinga, kwenye kongamano la uhamasishaji na uanzishwaji wa umoja  wa makandarasi na vikundi vinavyotumia teknolojia stahiki ya nguvu kazi katika ujenzi, ukarabati wa matengenezo ya barabara uliofanyika mkoani Mbeya katika Chuo cha Teknolojia Stahiki ya Nguvu Kazi (ATTI) na kuhudhuriwa na wakandarasi wadogo wadogo zaidi ya 150.

Arch. Mwakalinga, alisema kuwa Wizara kupitia taasisi zake zinazotekeleza miradi ya ujenzi itaendelea kutumia sheria na kanuni zilizowekwa ili kuhakikisha kazi zilizoainishwa kwenye miradi ya ujenzi ikiwemo ukarabati  na matengenezo ya barabara, madaraja na majengo zinafanywa na makandarasi  hao.

"Wizara imeteua timu ya wataalam kupitia nyaraka mbalimbali za miradi ya ujenzi ili kuhakikisha asilimia 30 ya fedha zinazolipwa kwenye mikataba mbalimbali ya ujenzi zinaelekezwa kwa makandarasi wanaotumia teknolojia ya nguvu kazi", alisema Mwakalinga. 

Aliongeza kuwa upitiaji utafanyika kwa haraka chini ya wataalam hao ambapo anaamini watafanya kazi hiyo vizuri ili kubainisha vigezo ambavyo makandarasi hao wamekuwa wakivilalamikia kila siku katika utekelezaji wa kazi zao ili vifanyiwe kazi.

Aidha Arch. Mwakalinga, alibainisha kuwa Serikali inatambua makandarasi hao ni chachu kubwa katika kutatua tatizo la ajira kwa wananchi hususani maeneo ya vijijini kwani mara nyingi wakandarasi hao hutumia vifaa na vibarua wanaopatikana katika eneo la mradi. 

"Mbali na kuongeza ajira na kuimarisha usafiri hususani maeneo ya vijijini, serikali inaelewa fika mnachangia kwa kiasi kikubwa uchumi wa nchi kwa kodi mnayolipa kupitia kazi mnazozifanya" alisisitiza Mwakalinga.

Alisema ni jukumu la wakandarasi hao kushirikiana na kufanya kazi kwa pamoja na kuwa na sauti moja katika kufuatilia fursa mbalimbali na maslahi yao na kupata ufumbuzi wa pamoja wa changamoto zinazowakabili. 

Awali akimkaribisha Katibu Mkuu huyo Mkurugenzi wa Barabara, Mhandisi Rogatius Mativila, alisema madhumuni ya kikao kazi hicho ni kujadili kwa pamoja masuala muhimu katika Sekta ya Ujenzi ili kuendeleza na kuimarisha matumizi ya Teknolojia ya Nguvukazi katika kutekeleza matengenezo ya barabara, madaraja na majengo bila kusahau sekta nyingine nchini. 

Akiongea kwa niaba ya makandarasi hao, Bi Aurelia Mtui, alitoa shukrani za dhati kwa Serikali kwani amekuwa kwenye taaluma hiyo kwa miaka 18 na kwa mara ya kwanza wamekutana na Katibu Mkuu  wa Sekta ya Ujenzi kuzungumzia changamoto zao na kuomba maazimio waliyokubaliana katika kikao hicho yafanyiwe kazi. 

Serikali ilianzisha mpango wa kuendeleza matumizi ya teknolojia ya Nguvukazi tangu mwaka 2004 na kulingana na takwimu zilizopo hadi kufikia mwezi Juni 2019 jumla ya Makandarasi 267 walikuwa wamesajiliwa na bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB) katika madaraja ya kutumia teknolojia ya nguvukazi.
 Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Arch. Elius Mwakalinga, akifungua kongamano la uhamasishaji na uanzishwaji wa umoja  wa makandarasi na vikundi vinavyotumia teknolojia stahiki ya nguvu kazi katika ujenzi, ukarabati wa matengenezo ya barabara lililofanyika katika Chuo cha Teknolojia Stahiki ya Nguvu Kazi (ATTI) mkoani Mbeya.
 Mshiriki wa kikao kazi cha Makandarasi wanaotumia teknolojia stahiki ya nguvukazi katika ujenzi, ukarabati na matengenezo ya barabara, Bw. Ambakisye Mwakipesile, akiwasilisha hoja zake kwa Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Arch.Elius Mwakalinga (hayupo pichani) katika kongamano lililofanyika katika Chuo cha ATTI Wilayani Rungwe Mkoani Mbeya na kushirikisha wakandarasi hao kutoka nchi nzima.
 Mkandarasi Boniface Mambya, akitoa maoni yake kwa Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Arch.Elius Mwakalinga (hayupo pichani) wakati wa kongamano la umoja kwa makandarasi na vikundi vinavyotumia teknolojia stahiki ya nguvu kazi katika Ujenzi ukarabati wa Matengezo ya barabara lililofanyika katika chuo ATTI, Mkoani Mbeya.
Washiriki wa kongamano la uhamasishwaji wa uanzishwaji wa umoja wa makandarasi na Vikundi vinavyotumia teknolojia stahiki ya nguvu kazi katika ujenzi, ukarabati wa matengezo ya barabara wakipitia baadhi ya makabrasha na kumsikiliza Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Arch.Elius Mwakalinga (hayupo pichani) lililofanyika katika Chuo cha ATTI, Mkoani Mbeya.