Mabaki ya mwili wa Naomi Marijani anayedaiwa kuuwawa na mume wake, kisha mwili wake kuchomwa moto na mabaki kufukiwa shambani, yamefikishwa kwenye Ofisi ya Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa lengo la kufanyia uchunguzi wa sampuli za mabaki hayo.

Mkemia Mkuu wa Serikali Dkt. Fidelice Mafumiko, amesema wameyapokea mabaki ya mwili huo na kwamba uchunguzi wa vinasaba katika sampuli hizo imeanza Julai 24.

Dkt. Mafumiko ameongeza kuwa, uchunguzi wa namna hiyo huchukua takribani siku 21, lakini watazifanyia kazi sampuli hizo ndani ya muda mfupi na kwa weledi mkubwa, na kwamba sampuli zinazohusisha mahakama na mauaji majibu yake hutoka haraka ili taratibu zingine ziendelee.

Tangu taarifa za kuuawa kwa Naomi zijulikane, ndugu wa marehemu imewabidi kusubiri majibu rasmi ya vinasaba yatakayothibitisha kama ni kweli yale ni mabaki ya ndugu yao ili waweze kuendelea na taratibu za msiba.

Inadaiwa kuwa Naomi aliuwawa Mei 15, 2019 na mume wake Khamis Luwongo kisha kumchoma na moto wa magunia mawili ya mkaa na kwenda kuyafukia mabaki hayo shambani kwake Mkuranga, ambapo hadi sasa Jeshi la Polisi linaendelea kumshikilia mwanaume huyo kwa upelelezi zaidi.