Nahodha wa timu ya taifa ya Tanzania Mbwana Samatta amebainisha kuwa amejaribu kuwatembelea gerezani viongozi wa zamani wa klabu ya Simba ambao ni makamu wa Rais Godfrey nyange 'kaburu'  na Rais wa TFF, Jamali Malinzi lakini hakufanikiwa kuwaona.

Samatta ambaye alikuwa na Taifa Stars nchini Misri ilikokuwa ikishiriki AFCON 2019 na kutolewa hatua ya makundi amesema licha ya kutowaona lakini anawaombea.

Kupitia Twitter Samatta ameandika, ''Leo nimebahatika kupita gereza la keko ili kuwaona ndugu Godfrey Nyange 'Kaburu' na ndugu Jamal Malinzi, lakini sikufanikiwa kuonana nao kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo'', amesema.

Samatta ameongeza kuwa ''Bado naendelea kuwaombea wao na wafungwa wote, amani na furaha''.

Kikosi cha Taifa Stars kilirejea jana kutoka nchini Misri ambapo kilicheza mechi tatu za Kundi C dhidi ya Senegal, Kenya na Algeria lakini kikapoteza mechi zote.