Dar es Salaam. Mwanahawa Abdul maarufu ‘Queen Darleen’ amesema anaamini uwezo wake, na hatishwi na msanii yeyote wa kike.

Darleen ambaye ni msanii pekee wa kike katika lebo ya WCB, amesema hayo baada ya kuulizwa na Mwananchi leo Ijumaa Julai 26, 2019 kuwa hahofii lebo hiyo kuongeza wasanii wakiwemo wa kike wenye uwezo.

Mwananchi ilitaka kujua hilo kutoka kwa Darleen baada ya uongozi wa lebo hiyo kwa nyakati tofauti kueleza mpango wa kusajili wasanii wengine ikiwamo wa kike.

Katika majibu yake, msanii huyu ambaye anatesa na kibao cha ‘Muhogo’  amesema suala hilo halijawahi kumuumiza kichwa kwa sababu anaamini anachokifanya.

“Siwezi kunung’unika msanii mwingine kusajiliwa kwenye lebo yetu wakiwamo wa kike kwa sababu hawanitishi ninajua ninachokifanya.”

“Isitoshe kila mmoja anataka kupata riziki, lakini ukisema nitapata taabu hapana nipo fiti kimuziki, ”amesema Darleen.

Mwananchi