ALIYEKUWA mshambuliaji wa Simba, Mganda, Emmanuel Okwi juzi jioni amewaaga rasmi wachezaji wenzake aliokuwa nao katika kikosi cha Simba msimu uliopita huku pia akiwaachia ujumbe mzito.Okwi ambaye msimu uliopita aliitumikia Simba kwa mafanikio makubwa na kuiwezesha kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara lakini pia kufika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, msimu ujao hatakuwa tena na kikosi hicho.Okwi anadaiwa kujiunga na Klabu ya Fujairah FC ya Falme za Kiarabu (UAE) hivi karibuni baada ya mkataba wake wa Simba kumalizika na alipotakiwa kuongeza alidaiwa kugoma kutokana na maslahi kuwa kidogo.Habari za kuaminika kutoka ndani ya Simba ambazo Championi Ijumaa limezipata, zimedai kuwa, juzi Jumatano Okwi aliwaaga wachezaji wenzake kwa njia ya ujumbe alioandika katika ‘group’ la WhatsApp la wachezaji hao.“Jana, Jumatano (juzi), Okwi ametuaga na kutuambia kuwa anaenda kujiunga na timu ya Fujairah ya Falme za Kiarabu kwa hiyo anatutakia kila la heri katika msimu ujao wa ligi kuu.“Ametuambia tumeishi naye vizuri lakini ameamua kuondoka Simba siyo kwa ubaya bali ni kwa ajili ya kutafuta maisha kama ambavyo wachezaji wengine wamekuwa wakifanya pindi wanapopata sehemu yenye maslahi mazuri.“Kwa hiyo Fujairah wamempatia mzigo wa kutosha, ndiyo maana ameamua kujiunga nao, hata hivyo ametuambia kuwa tuna deni kubwa ambalo tunadaiwa na Simba ambalo tunatakiwa kuhakikisha tunalilipa.“Ametuambia kuwa msimu ujao tunatakiwa kupambana kwelikweli ili kuhakikisha tunatetea ubingwa wetu wa ligi kuu lakini pia kufika hatua ya nusu fainali katika Ligi ya Mabingwa Afrika,” alisema mchezaji huyo ambaye aliomba kutotajwa jina lake. Alipotafutwa Okwi kwa njia ya simu ili aweze kuzungumzia hilo, hakupatikana.

Sweetbert Lukonge, Dar es Salaam