OFISA Mtendaji Mkuu wa klabu ya Simba SC,  Crescentius Magori,  leo Julai 16, 2019,  amefunguka kwamba wameletewa barua ambayo inadhihirisha kuwa  Hamisi Kilomoni kavuliwa udhamini wa klabu Simba ya jijini Dar es Salaam.

Magori ameyasema hayo akizungumza na vyombo vya habari alipoongeza kuwa mzee huyo anafanya makusudi ya kuichafua klabu hiyo na ndiyo maana uongozi umeamua kuliweka wazi jambo hilo wazi.

“Alikoma udhamini wa Simba tangu Oktoba 2017, ambapo Novemba 8 alijulishwa kupitia wakili wake kuwa yeye siyo mdhamini wa Simba,” alisema Magori.

Katika siku za hivi karibuni, baada ya klabu hiyo kuanza kujiendesha kibiashara kufuatia mfanyabiashara Mohamed Dewji (Mo) kuwekeza katika klabu hiyo, kumekuweko na mgogoro wa chinichini baina ya uongozi wa klabu hiyo maarufu ya Dar es Salaam na mchezaji wa zamani wa klabu hiyo, mzee Hamisi Kilomoni.