Wabunge Kwenye kikao, watimua mbio
Wabunge katika eneo la Kusini Magharini mwa Jimbo la Ondo nchini Nigeria, walilazimika kukatisha kikao chao na kutimua mbio baada ya nyoka kuanguka ndani ya ukumbi kutoka kwenye paa la jengo hilo, Alhamisi, Julai 25, 2019.

Kwa mujibu wa gazeti la Premium Times la nchini humo, nyoka huyo alitokea kwenye tundu la paa, hali iliyozua taharuki na hofu miongoni mwa wabunge na watu waliokuwa wanashiriki kikao hicho.

Hata hivyo, kwa mujibu wa wabunge hao, hakuna aliyejeruhiwa au kung’atwa na kwamba nyoka aliuawa na kuchomwa moto.

“Ule ukumbi sio salama tena kwa kufanyia vikao vya wabunge. Kwa sababu hiyo, tumeamua kuondoka mara moja kuhamia sehemu nyingine,” alisema Mbunge Olughenga Omole alipozungumza na Premium Times.

Zoezi la kupuliza dawa (fumigation) kwa lengo la kuwaondoa wadudu na wanyama hatari ndani ya jengo hilo limepangwa kuanza leo ili wabunge warejee siku za usoni kwenye ukumbi huo.

Hilo sio tukio la kwanza barani Afrika mwaka huu kwa nyoka kuvamia maeneo ya kazi ya viongozi. Aprili mwaka huu, nyoka aliripotiwa kuonekana kwenye ofisi ya Rais wa Liberia, George Weah na kumlazimisha kuhama ofisi hiyo kwa muda kupisha zoezi la kupuliza dawa na kuondoa wadudu hatari.