WAZAZI, walezi na walimu wametakiwa kushirikiana kwa pamoja ili kufanikisha wanafunzi waanze wakiwa wadogo kutumia akili zao ipasavyo kwa kutatua matatizo yao kwa sasa ili miaka ijayo wakiwa wakubwa waweze kuwa wabunifu na kufanya maendeleo.
Katibu wa bodi ya shule ya awali na msingi New Light ya Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Oscar Gunewe aliyasema hayo juzi wakati akizungumza na wazazi na walezi wa wanafunzi wa shule hiyo.
Gunewe alisema watotot wanapaswa kupewa nafasi na kukuzwa kiakili kwa kutakiwa kufundishwa kujiamini na kutumia akili zao kutatua changamoto walizonazo ili wakiwa wakubwa wasishindwe kuyatatua.
"Nchi zilizoendelea wanasema sisi wa Afrika hatutumii akili zote tulizonazo katika kufikiri, hovyo yatupasa kuwajenga watoto katika msingi wa kutumia akili zao kwa asilimia zote wakiwa wadogo katika kifikiri, alisema.
Alisema maendeleo ya miaka ijayo ya nchi ya Tanzania inawategemea watoto, kutokana na hali hiyo hayo yatakwama bila kujengwa msingi imara katika malezi, makuzi na masomo bora hivi sasa.
Mwalimu mkuu wa shule hiyo ya awali na msingi New Light, Tumaini Mbise alisema wanajivunia shule hiyo kwani ina walimu wazuri wanaofundisha ipasavyo hivyo wazazi na walezi wasiwe na hofu pindi wakiwaleta watoto wao.
Mbise alitoa mfano wa mwanafunzi wa darasa la tatu wa shule hiyo ambaye alishindikana jijini Arusha akiwa darasa la pili kutokana na utukutu lakini wakaweza kumrudisha akawa na nidhamu.
"Siku ya kwanza alipofika hapa shuleni sisi walimu tulichoka kwani alikuwa mtundu mara apande juu ya mti, lakini tuliweza kukaa naye na kumpa ushauri bila kumchapa na sasa ni mtoto mwenye nidhamu na bidii ya masomo," alisema.
Mmoja kati ya wazazi mwenye watoto kwenye shule hiyo Happy Kayumbo aliwaomba wazazi na walezi kutoa ushirikiano kwa walimu wa shule hiyo ili waweze kutimiza wajibu wao ipasavyo katika kuwafundisha wanafunzi.
Kayumbo alisema baadhi ya wazazi na walezi huwa hawafiki shuleni kujua maendeleo ya watoto wao hivyo wanapaswa kufika na wasisubiri hadi waitwe kwenye vikao.
Wanafunzi wa darasa la sita wa shule ya awali na msingi New Light Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkpani Manyara wakiwa kwenye kikao cha wazazi, walezi na walimu wao.
Wanafunzi wa darasa la tatu wa shule ya awali na msingi New Light wakiwa kwenye kikao hicho cha wazazi, walezi na walimi wao.
Mmoja kati ya wazazi wa wanafunzi wa shule ya awali na msingi New Light ya Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara akiwa na mwanafunzi aliyepata zawadi ya kuwa wa kwanza katika darasa lake.