Mtoto wa miaka 10 Aieleza Mahakama Jinsi Baba wa Kambo Alivyomnyonga Mama Yake Hadi Kufa
Mtoto mwenye umri wa miaka 10, jina (limehifadhiwa) ameisimulia Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jinsi alivyoshuhudia  baba yao wa kambo, Godfrey Samweli au Nkwabi akimnyonga mama yake Bahati Hussein na kimsababishia kifo.

Mtoto huyo anayesoma darasa la tatu, juzi Julai 3/2019 ameeleza mbele ya Msajili wa Mahakama Kuu, Pamela Mazengo kuwa alishtuka usingizini wakati wa usiku na kumshuhudia baba yao akimkunja shingo mama yake kama anaivunja na kumwambia asipige kelele.

Akiongozwa na Wakili wa Serikali, Erick Shija, kutoa ushahidi  wake dhidi ya kesi ya mauaji inayomkabili Godfrey, mtoto huyo ambae ni shahidi wa tatu kati ya mashahidi watano waliotoa ushahidi leo, amedai mama yake amefariki mwaka 2014.