Mkurugenzi Mkuu wa Shirikisho la Korosho Barani Afrika, Ernest Mintah (kulia) akifafanua jambo na wanahabari juu ya mkutano mkuu wa 13 wa wadau wa Korosho Afrika unaotarajia kufanyika jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirikisho la Korosho Barani Afrika, Ernest Mintah (kulia) akizungumza na wanahabari juu ya mkutano mkuu wa 13 wa wadau wa Korosho Afrika unaotarajia kufanyika jijini Dar es Salaam. Katikati ni Dkt. Steven Ngailo wa Wizara ya Kilimo. Picha na Cathbert Kajuna - Kajunason/MMG.
Dkt. Steven Ngailo wa Wizara ya Kilimo akizungumza jambo.

Na Leandra Gabriel, Blogu ya jamii.

MKUTANO mkuu wa 13 shirikisho la wadau korosho Afrika (ACA) linatarajiwa kufanyika nchini kwa siku 3 kuanzia tarehe 7-9 Novemba 2019 jijini Dar katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC) huku mada ya mkutano kwa mwaka huu ikiwa ni; “Kuendeleza Ushirikiano na Kushawishi Mabadiliko katika Soko”.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mkuu wa Shirikisho la Korosho Barani Afrika, Ernest Mintah amesema kuwa mkutano huo umelenga kutathimini mabadiliko katika soko, mwitikio wa serikali na watendaji wanaotengeneza mnyororo wa thamani na kuchanganua wajibu wa wadau wote katika kushughulikia masuala yanayojitokeza.

Amesema kuwa mkutano wa mwaka wa Korosho wa ACA kwa mwaka huu umekuwa ni tukio kubwa sana la korosho Afrika ambalo litawakutanisha wadau wa tasnia mbalimbali za korosho kutoka duniani kote ambapo siku tatu za mkutano huo wakulima, wafanyabiashara, wabanguaji, wasafirishaji, viongozi wa serikali, watengenezaji wa vifaa, na watoa huduma watakutana ili kuzungumza na kujadili mwelekeo, changamoto na fursa.

Kwa upande Dkt. Steven Ngailo kutoka Wizara ya Kilimo amesema kuwa mkutano huo utawakutanisha washiriki na wataalamu wa korosho zaidi ya 500 na kujadili masuala hasa taarifa sahihi kufika kwa wadau na wakulima kwa wakati.

Ngailo amesema kuwa Afrika imekuwa kinara katika uzalishaji wa korosho katika soko la dunia huku Tanzania ikishika nafasi ya pili licha ya kuwepo kwa changamoto za uwepo wa viwanda vya ubanguaji.

Imeelezwa kuwa mkutano huo unategemewa kuleta tija kwa wadau na wakulima na korosho huku nchi wanachama zikishauriwa kushirikiana, kuvutia wawekezaji na umoja huo uende kwenye mazao mengine kwa kuunda mashirikisho ya namna hiyo.