Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam nchini Tanzania, Paul Makonda amepiga marufuku 'watu wachafu' kuonekana mitaa ya mjini ya jiji hilo katika kipindi cha mkutano wa wakuu wa nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Mkutano huo wa 39 wa SADC unatarajiwa kufanyika mwezi ujao, Agosti 18 na 19.

Kama sehemu ya maandalizi ya mkutano huo, Bwana Makonda amesema jiji hilo leye wakaazi wengi zaidi nchini Tanzania litakuwa katika hali ya usafi mkubwa.

"Tabia ya kuja mjini bila kunyoosha nguo ni marufuku. Tabia ya kuja mjini hujaoga ni aibu. Watu wanatembea tu na chawa, kama huwezi kuwa msafi basi subiri mwezi huu upite," Makonda amenukuliwa na gazeti la Mwananchi la nchini humo akisema na kuongeza: "Kwa kipindi hiki tuvumiliane, kama hufui nguo, kama huogi, pumzika kidogo kuja mjini."

Sababu ya kutoa amri hiyo kwa mujibu wa Makonda ni kuepuka "kumtia aibu Rais wa Tanzania John Magufuli mbele ya marais kutoka nchi 15 watakaokuwa hapa nchini."

Pia, Makonda ameagiza kwamba mtu yoyote mwenye gari atakayetupa takataka barabarani asitozwe faini badala yake apewe eneo la kufanya usafi. Amesema baadhi ya watu hao wana jeuri ya fedha, hivyo kwao faini siyo adhabu.

Dar es Salaam ndio jiji lenye watu wengi zaidi Tanzania na linaongozwa na Paul Makonda
"Mtu mwenye gari akitupa takataka msimtoze faini, mshusheni kwenye gari, mpeni kipande cha kilomita moja cha barabara apige deki. Hawa watu fedha kwao siyo tatizo, sasa tunataka kuwaonyesha kwamba na sisi tuko 'serious' na usafi wa jiji letu."

Makonda ambaye ni moja ya viongozi walio karibu na rais Magufuli si mgeni masikioni mwa Watanzania kwa kutoa maagizo ambayo huacha watu wazi.

Hivi karibuni alitangaza operesheni dhidi ya wapenzi wa jinsia moja jijini humo hali iliyopelekea Tanzania kuingia katika wakati mgumu na baadhi ya mataifa ya magharibi.

Makonda pia alijiingiza katika mgogoro wa waziwazi na mamlaka ya kukusanya kodi nchini humo (TRA) na Waziri wa Fedha Philip Mpango kwa kutaka mzigo wake wa samani za shule kupitishwa bandarini kwa msamaha wa kodi.

Mzozo huo uliisha baada ya rais Magufuli kumkanya na kumtaka alipe kodi mara moja.

Shughuli za usafi katika jiji hilo kwaajili ya mkutano wa SADC zinatarajiwa kuanzia leo kuendeshwa na vijana 130 wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na mgambo 300 katika maeneo mbalimbali ya jiji.