Serikali ya Marekani imeidhinisha adhabu ya kifo ianze tena kutekelezwa, baada ya adhabu hiyo kusitishwa miaka 16 iliyopita, ambapo imehalalishwa kisheria katika majimbo 29 nchini humo.

Katika taarifa iliyotolewa na mwanasheria mkuu wa nchi hiyo, William Barr amesema kuwa tayari ameiagiza Halmashauri ya Magereza, kupanga siku ya kunyongwa kwa wafungwa watano waliopewa adhabu hiyo, ambao walishtakiwa kwa kuhusika na mauaji na ubakaji wa watoto na watu wazima na hukumu yao imepangwa kutekelezwa Disemba 2019 na Januari 2020.

Aidha, mwanasheria huyo ameiagiza Halmashauri ya Magereza,  kubuni sera itakayoidhinisha matumizi ya dawa moja kwaajili ya kumuua mtu, badala ya kutumia aina tatu za dawa ambayo ilikuwa ikitumika hapo mwanzo

Adhabu ya kifo ilitekelezwa mara ya mwisho mwaka 2003 dhidi ya Louis Jones Jr (53), mbabe wa vita vya Ghuba aliyemuua askari wa miaka 19 Tracie Joy McBride.

Kwa mujibu wa taarifa zilizokusanywa na kituo kinachonakili taarifa kuhusu adhabu ya kifo, watu 78 walihukumiwa adhabu ya kifo kati ya mwaka 1988 na 2018,  lakini ni watu watatu tu kati ya hao waliouawa.