Kwa kutambua mchango wa Sekta za Kilimo, Mifugo na Uvuvi katika kuinua uchumi wa Tanzania, Wakuu wa Mikoa ya Simiyu, Mara na Shinyanga kwa kushirikiana na Mawaziri wenye dhamana ya Kilimo, Uvuvi na Ufugaji wanawakaribisha Wakulima, Wafugaji, Wavuvi na Wadau wengine kwenye maonesho na maadhimisho ya sikukuu ya Nanenane Kitaifa yatakayofanyika katika Viwanja vya Nyakabindi, Bariadi Mkoani Simiyu kuanzia tarehe 28/07/2019 na kilele chake kuwa tarehe 08/08/2019.

Ufunguzi rasmi wa Maonesho hayo utafanywa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan siku ya tarehe 01/08/2019. Kaulimbiu ya Nanenane mwaka huu ni “Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa ukuaji wa Uchumi wa Nchi”.

Wakati wa maadhimisho hayo, tarehe 03/08/2019 itakuwa siku ya “Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDP ll)” Mgeni rasmi atakuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Kasimu Majaliwa Majaliwa, siku ambayo wananchi watajenga uelewa zaidi kuhusu utekelejazi wa “Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili’

Mgeni Rasmi siku ya kilele ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. Kutakuwa pia na mafunzo ya nadharia na vitendo kwa Wakulima, Wafugaji na Wavuvi ili kuongeza uzalishaji na tija. Sambamba na hiyo kutakuwa na kongamano kuhusu namna bora ya kuendesha kilimo biashara, teknolojia mpya, masoko na mitaji.

KARIBUNI KANDA YA ZIWA MASHARIKI ili kuona fursa mbalimbali zitakazomwezesha mwananchi kuinua uchumi wake binafsi na Taifa kwa ujumla