PANAPOKUCHA watu wanaelekea kazini, watoto shuleni. Vyombo vya usafiri wa umma na binafsi vinachoma mafuta kuwapeleka panapohusika.

Kazini zinatafutwa fedha ili kuyashinda maisha. Shuleni watoto wanapikwa wawe tabaka bora. Njiani utakutana na ombaomba, wanahitaji kusaidiwa wayamudu maisha.

Watoto wengine wapo shule, wengine barabarani wanaomba. Wanaosoma, wengine wapo shule za kifahari, wengine hohehahe, ilimradi wino wa kalamu unapita kwenye daftari. Watoto wote wanaifikiria kesho yao njema!

Watu wanaitumia bahari kwa mazoezi. Wengine starehe. Wapo wanaitumia kusaka fedha. Bahari ni miundombinu asilia kutoka nchi kwenda nchi, kisiwa kwa kisiwa.

Anayejenga nyumba anatumia fedha, wajenzi wanaingiza fedha. Wa zege, wanavunja kokoto. Viwanda vinafurika watu. Barabarani wamachinga wanafanya yao.

Wanamuziki wanaburudisha wanaoishi. Waigizaji wanaigiza kuishi. Kumbi za starehe watu wanakula raha, wengine ni sehemu ya kusaka pesa.

Usikasirishwe na usumbufu wa wapiga debe kwenye vituo vya mabasi, wanasaka maisha. Hata ndege zina wapigadebe, abiria anachanwa msamba kwa kuvutwa huko na kule.

Yupo anayeamini uinjinia, mwingine udaktari, yupo rubani, vipi nahodha wa meli? Hao wanalipwaje bila mhasibu? Wachumi, wanasheria, walimu, wafanyabiashara, waandishi wa habari, kila mmoja na jukwaa analoliamini.

Maisha yana utajiri wa fursa. Yana milango elfu ya mafanikio. Huoni waliokuwa hamnazo shuleni wanatajirika na kuajiri wasomi? Hushangai wenye ulemavu wanaajiri wanaojiona wamekamilika?

Maisha hayajawahi kumkatili mtu. Ukiyaamini na kuyawaza kwa upendo, yatakushangaza kwa fursa ambazo yatakupa. Uwe mlemavu, huna elimu au afya mgogoro.

Ukiujua ukweli kuhusu maisha na Mungu, hutakata tamaa. Hutaacha kufurahia maisha hata kama ni magumu.

Thomas Edison, kiziwi aliyefukuzwa shule kisa hafundishiki, alitafuta maarifa kwa kusoma vitabu. Huyohuyo ndiye mgunduzi na mtengenezaji wa kwanza wa kifaa cha kurekodia sauti na kamera za video.

Milango hufungwa lakini mingine ipo wazi. Ukifukuzwa kazi, zipo nyingine. Huna elimu, kuna fursa. Unajiona una upungufu, lipo jambo unalimudu kuliko wote. Maisha yamejaa ukarimu. Usiwe mnyonge.

Ndimi Luqman MALOTO