Uganda imelezea hofu yake kuhusu hali ya raia wa nchi hiyo wanaofanya kazi Oman ikidai kuwa huenda ni wahanga ''ulanguzi'' wa binadamu.

Suala hilo limeangaziwa katika ripoti iliyowasilishwa bungeni leo Ijumaa.

Zaidi ya Waganda 40,000 wanafanya kazi Oman - taifa ambalo halina makubaliano yoyote ya kibiashara.


Serikali ya Uganda imekuwa ikijaribu kuwafikia raia wake ambao ni wahamiaji wanaofanya kazi Mashariki ya Kati baada ya kupokea simu za kutafuta usaidizi kutoka kwa raia hao wanaofanya kazi za ndani.

Wengi wao ni wanawake ambao wamekosa nafasi ya ajira chini mwao na kuamua kutafuta kazi katika mataifa ya Uarabuni.

Lakini mpango wa ajira kwa wahamiaji umekumbwa na madai ya unyanyasaji wa kingono pamoja na dhulma wanazopitia wafanyikazi wa ndani kutoka kwa waajiri wao.

Haki miliki ya pichaDAILY MONITOR
Wengi wao wamekuwa wakinasa kanda za video na kuzisambazwa katika mitandao ya kijamii wakiomba jamaa na marafiki wawasaidie kurudi nyumbani.

Katika kisa cha hivi karibuni mwanamke wa umri wa makamo waliyekuwa akifanya kazi Jordan, alidai kuuzwa kama mtumwa kwa dola 3000.

Alimpigia simu mbunge mmoja nchini Uganda ambaye baadae aliwasilisha kisa chake katika bunge la nchi hiyo.

Licha ya changamoto zinazowakabili raia wake ugenini, serikali ya Uganda imesema kuwa haitasitisha mpango wa kuwapeleka watu wake kufanya kazi nje ya nchi.