Msanii wa Bongofleva mwanadada Lulu Diva, ameweka wazi uhusiano wake na msanii Jaguar, ambaye pia ni mbunge wa Jimbo la Starehe huko Kenya kwa kusema kuwa wawili hao ni marafiki wa muda mrefu.

Lulu Diva ameweka bayana hilo kwenye Friday Night Live ya East Africa Television ambapo amesisitiza kuwa yeye binafsi anamkubali Jaguar muda mrefu sana, lakini hajui kama mkali huyo ameoa au hajaoa, kwani wao wanashirikiana kikazi tu.

''Jaguar ni 'My Crush' muda mrefu sana na amenipa 'support' kubwa sana, urafiki wetu sidhani kama una mashaka sana kwasababu yeye ni mtu anayependa kuinua kila mtu mwenye kipaji na hakuna chochote kinaendelea kati yetu'', amesema.

Mrembo huyo ambaye amewahi kuonekana kwenye video mbalimbali za wasanii enzi hizo akiwa kama 'Video Vixen', ameongeza kuwa ni kweli wao walikuwa karibu sana wakiwa Kenya kwa siku tatu lakini Jaguar akakamatwa.

Lulu Diva amemaliza kwa kusema kuwa siku ambayo anarudi Bongo ndio siku Jaquar alitoka mahabusu, baada ya kushikiliwa kwa siku kadhaa kutokana na maneno yake yaliyodaiwa kuwa ya kichochezi dhidi ya raia wa nchi jirani ikiwemo Tanzania.