Mchana wa leo katika mchuano ya ICC Manchester United wanakutana na wenzao wa Ligi ya Uingereza majogoo wa jiji la London, Tottenham Hotspur mashabiki wategemee pambano la aina yake aisee.
Dimba la Hongkou jijini Shanghai ambalo linaweza kuchukua mashabiki 33,000 ndilo litakalowajibika kuhodhi mtanange huo Alhamisi ya leo.

Japokuwa ni wazi kwamba timu hizi zitachezesha wachezaji wasiokuwa na uzoefu sana na wasio na majina makubwa, mashabiki wa soka nchini China wako tayari kushuhudia mchezo huo.
Timu hizi mbili zinaingia katika mechi hiyo zikiwa zimetoka kupata ushindi katika mechi zao za kwanza, Manchester United waliifunga Inter Milan 1-0 huko Singapore Jumamosi iliyopita, huku Harry Kane akiifungia Spurs goli kutoka katikati ya uwanja na kuwapa ushindi wa 3-2 dhidi ya mabingwa wa Serie A Juventus.

Dhidi ya Juventus kocha wa Spurs Mauricio aliwapa nafasi wachezaji kama golikipa Paulo Gazzaniga, beki Anthony Georgiou na Japhet Tanganga, sambamba na kiungo Olivier Skipp na mshambuliaji mwenye miaka 17 Tory Parrott ambao walianza kwenye kikosi cha kwanza.
Kocha wa United Ole Gunnar Solskjaer alienda mbali zaidi, kwa kuanza mchezo dhidi ya Inter kwa mchanganyiko wa wachezaji wachanga na wale wenye uzoefu, na baadaye kuwabadilisha wachezaji wote 11 katika kipindi cha pili.

Kwa muda mwingi ni mchezaji aliyenunuliwa kwa dau la paundi Milioni 50 Aaron Wan-Bissaka ndiye aliyevutia zaidi kwa upande wa United, ambaye ndiye alikuwa nyota wa mchezo katika mechi yake ya tatu tu tangu ajiunge na United akitokea Crystal Palace.

Scott McTominay alisema kwamba mlinzi huyo mwenye miaka 21 ameingia na kufiti vizuri kwenye kikosi cha United. “Yuko kama wachezaji ambao wamekuwepo hapa kwa muda mrefu, ni vizuri kuwa naye pia ni mchezaji mkubwa ambaye atakuwa wa muhimu sana kwenye timu yetu.
“Inachukua muda mrefu kwa mchezaji mpya kuzoea lakini huyu amezoa mara moja”

Mchezo huo utapigwa majira ya saa nane na nusu (8:30) Mchana wa leo huko Shanghai China. Kwa mashabiki wa soka nchini watautazama kupitia king’amuzi cha StarTimes kwenye chaneli ya ST World Football HD.