Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo imethibitisha kisa cha kwanza cha Ebola katika mji uliopo mashariki Goma, ambapo kuna zaidi ya watu milioni moja wanaoishi.

Wizara ya afya imethibitisha kwamba mchungaji mmoja amekutikana kuwa na virusi vya ugonjwa huo baada ya kufanyiwa ukaguzi katika kituo kimoja huko Goma punde alipowasili kwenye basi jana Jumapili.

Wizara hiyo imesema nafasi ya kusambaa kwa ugonjwa huo ni ndogo.


Zaidi ya watu 1600 wamefariki kufikia sasa tangu kuzuka mlipuko wa Ebola mashariki mwa nchi hiyo mwaka mmoja uliopita.

Mchungaji huyo alisafiri umbali wa 200 km kutoka Butembo hadi Goma kwa basi, ambako alikuwa amekutana na watu wenye ugonjwa huo.

Katika taarifa yake wizara ya afya imesema: "Kutokana na kasi ambayo mgonjwa ametambulika na kutengwa, pamoja na kutambuliwa kwa abiria wengine wote kutoka Butembo, hatari ya kusambaa katika sehemu nyingine za mji wa Goma ni ndogo."


Je inawezekana kuangamiza virusi vya Ebola?
Imesema kuwa dereva wa basi hilo na abiria wengine 18 watapewa chanjo leo Jumatatu.

Wizara ya afya Goma imekuwa katika hali ya kujitayarisha kwa mlipuko wa ugonjwa huo. Mnamo Novemba mwaka jana iliidhinisha shughuli za utayarisho na muitikio wa iwapo mlipuko huo utatokea.

Maafisa 3000 wa afya mjini humo tayari wamepewa chanjo.

Mlipuko mkubwa wa Ebola ulishuhudiwa Afrika magharibi mnamo 2014- 2016 na uliahiri takriban watu 28,616 zaidi nchini Guinea, Liberia na Sierra Leone. Takriban watu 11,310 walifariki.

Ebola huwaathiri binaadamu kupitia mgusano na wanyama walioathirika kama tumbili, na popo wa msituni.

Ugonjwa huo unaweza kusambaa kwa kasi kupitia mgusoano wa kiwango hata kidogo cha maji wa mwilini ya waathirika au kwa kugusa maeneo yalio na majimaji ya mgonjwa muathirika.