Kipa mpya wa Yanga, Metacha Mnata, amefunguka kuwa anafurahi kupata nafasi ya kucheza timu moja na beki Kelvin Yondani kwa sababu ni mchezaji mkubwa na mwenye heshima hapa nchini na ilikuwa ni ndoto yake.

Metacha amesajiliwa na Yanga hivi karibuni kuzipa pengo la kipa wa timu hiyo, Beno Kakolanya ambaye ametimkia katika kikosi cha Simba kwa ajili ya msimu ujao.

Metacha alisema ilikuwa ni ndoto yake siku moja kuja kucheza na Yondani kutokana na heshima aliyojiwekea kwenye soka na hilo limetimia.

Metacha alisema ataendelea kushirikiana naye vyema kuhakikisha wanaisaidia Yanga kufanya vizuri. “Ni jambo zuri kwangu na ninafurahia sana na kuna wengine wanatamani kucheza na Yondani kutokana na ubora wake, ni mchezaji mkubwa na hakuna asiyejua heshima yake aliyojiwekea hapa nchini kutokana na kazi yake.

“Nafurahi kuona ndoto yangu inatimia ya kucheza na mtu kama yule, zaidi tu ni mimi kuweka bidii na kuhakikisha naisaidia timu yangu kufika mbali na kutimiza malengo ambayo tumejiweka na nitaendelea kupambana kuhakikisha nakuwa vizuri,” alisema Metacha