MSANII mkongwe katika tasnia ya muziki wa Bongo Fleva, Juma Kassim ‘Nature’ amefunguka kuwa, ana nyimbo nyingi alizofanya yeye mwenyewe na alizowashirikisha wasanii wengine ambazo bado hajaziachia.  Akizungumza na Star Showbiz, Nature alisema kuwa, watu wengi wanasema ametulia, hana jipya, lakini amewatoa hofu kuwa ana midundo mikali aliyofanya na amewashirikisha wasanii kama Nandy na Harmonize.

“Ndiyo, watu hawajui nina kazi ambazo nimefanya mimi na nyingine nimewashirikisha wasanii, nimefanya kazi na Nandy pia nimefanya na Harmonize, niwatoe hofu mashabiki, kuna kazi zinakuja muda mfupi ujao,” alisema Nature.

Aidha, Nature alifunguka kuwa hana mpango wa kutoa albamu kutokana na soko lenyewe kwa sasa kuanzia utayarishaji wake hadi ifike sokoni. “Kwa sasa sijafikiria kutoa albam japokuwa albam ninayo imeandaliwa na ipo studio, lakini sijafikiria kuitoa kutokana na changamoto ya soko lenyewe kuwa gumu,” alisema Nature. Nature ni mmoja kati ya wasanii wakongwe ambao waliweza kutikisa na ngoma kali ikiwemo Mugambo, Mtoto Idd, Mikikimikiki, Zali la Mentali aliyoshirikishwa na Profesa Jay