Jaji Mkuu Awataja Wanaochelewesha Kesi
Jaji Mkuu wa Tanzania Ibrahimu Juma, amesema kumekuwa na changamoto ya watuhumiwa kukamatwa wakati upelelezi haujakamilika na kwamba kitendo hicho ni kinyume kwani kinapelekea wafungwa kujaa magerezani.

Hayo ameyabainisha mara baada ya kuwaapisha mawakili ambapo amesema, tangazo lililotolewa na Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) mwaka 2012, linawataka wasikamate watu kabla ya upelelezi kukamilika.

Aidha, Jaji Mkuu amesema kumekuwa na changamoto za upelelezi kutumia muda mrefu, kukamilika hivvyo wapelelezi wanatakiwa kulaumiwa na sio mahakama.

"Watu wa kulaumiwa hasa ni wapelelezi na sio mahakama, upelelezi unachukua muda mrefu na sababu wanazozitoa mahakamani, hazina mashiko, sisi tunataratibu zetu ambazo DPP alishazitoa katika tangazo la mwaka 2012," amesema Jaji Mkuu.

Na kuongeza kuwa, ''tangazo linasema usimkamate mtu kabla ya upelelezi kukamilisha, bahati mbaya hilo halifuatwi watu wanawakamata ndipo upelelezi unaanza inachangia kuongeza wafungwa gerezani," alisema Jaji Mkuu.