Instagram inaficha idadi ya 'likes' kwenye posti zinazowekwa katika nchi kadhaa, ili kuondoa hali ya ushawishi kwa watumiaji.

Majaribio ambayo yanaanza siku ya Alhamisi, hii ikimaanisha kuwa watumiaji wataona jina la mtumiaji wa anuani na chini ya picha zilizowekwa hawataona idadi ya waliopenda picha hizo.

Imeelezwa kuwa mitandao ya kijamii inaweza kuchangia hali ya 'kutojiamini' na pia vijana kujiona 'hawafai'.

Instagram imefanya majaribio katika nchi ya Canada mwezi Mei na majaribio mengine yanafanyika Australia, New Zealand, Ireland, Italy, Japan na Brazil, Kampuni hiyo imeiambia BBC.

Dawa ya wadhalilishaji mtandaoni inakuja

Kampuni ya Facebook yakiri kukabiliwa na matizo ya kiufundi

''Tuna matumaini kuwa jaribio hili itaondoa hali ya wasiwasi wa kutaka kujua idadi gani ya watu waliopenda kilichowekwa kwenye mtandao huo, hivyo watu wataweka vitu vyao vile wapendavyo wao,'' Mia Garlick mtaalamu kutoka Facebook Australia na mkurugenzi wa masuala ya sera nchini New Zealand ameeleza.

Nia ya kutekeleza hatua hii ni kuwafanya watumiaji wasione wanahukumiwa na kuona ''kama mabadiliko haya yatawasaidia watu kutojali kuhusu kupendwa kwa wanachokiweka mtandaoni''.

Instagram imesema kuwa jaribio hilo halitaathiri mfumo wa tathimini kwa ajili ya biashara. Na watumiaji bado wataweza kuona orodha ya watu waliopenda kilichowekwa mtandaoni kwa kubofya kwenye picha hiyo.

Wakati jaribio lilipokuwa likifanyika Canada instagram ilisema nia ilikuwa kupunguza mashinikizo ambayo yalifanya watumiaji kushindana mtandaoni ili wanachokiwekwa kipate idadi kubwa ya 'likes'

''Tunataka watu waondoe hofu kubwa kuhusu wapata 'likes' ngapi bali wapate muda wa kuungana na marafiki wanaowajali''. Alieleza afisa wa juu wa kampuni ya Instagram Adam Mosseri wakati ambapo idadi ya 'likes' kwenye kinachowekwa kimekuwa kipimo cha mafanikio na umaarufu kwenye mtandao huo.

Tafiti zinaeleza kuwa mrejesho wa papo hapo kuhusu kinachowekwa mtandaoni kinawafanya watu waendelee kujiamini lakini pia zimewafanya wengine kujiona hawafai ikiwa hawapati mrejesho wa kuridhisha.

Tafiti zimehusisha mitandao ya kijamii na athari za afya ya akili, hasa kwa vijana.

Idadi ya 'likes' ni njia pia ya kuweka thamani ya kitu kilichowekwa mtandaoni kwa upande wa kibiashara ndani ya Instagram.

Watu wenye ushawishi ambao hulipwa kwa ajili ya yale wanayoyaonesha hupimwa kwa idadi ya watu walichopenda kilichowekwa nao katika mitandao ya kijamii.

Mwanzoni mwa mwezi huu Instagram ilitangaza kuwa na mfumo mpya wa kukomesha udhalilishaji kwenye mtandao wake.