Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) Jumatatu, Julai 15, 2019 imeanza kuendesha programu za elimu kuhusu uombaji mikopo kwa wanafunzi waliomaliza kidato cha sita mwaka huu ambao wapo katika kambi 17 za Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) nchini kote.

Programu hizo ni muendelezo wa programu za elimu ya uombaji mikopo kwa usahihi ambazo HESLB iliziendesha mwezi April na Mei mwaka huu katika shule 119 za sekondari zilizopo kwenye mikoa 17 na kuwafikia wanafunzi 27,913 waliokua wanajiandaa na mitihani ya kitaifa ya kidato cha sita iliyomalizika mwishoni mwa mwezi Mei mwaka huu.

Akizungumza katika kambi ya JKT Ruvu Jumatatu, Julai 15, 2019 Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Bw. Abdul-Razaq Badru amesema lengo la programu hizo ni kuwawezesha wanafunzi kuomba mikopo kwa usahihi na hatimaye wenye sifa wapate mkopo na elimu ya juu.

“Kwa kushirkiana na wadau wetu, likiwemo Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), tumedhamiria kuwafikia wahitaji wa mikopo pale walipo, ndiyo sababu tupo hapa na wenzetu wapo katika kambi nyingine kama 16 ... na ikumbukwe tuliendesha programu kama hizi katika shule ya sekondari Tanzania Bara na Zanzibar,” amesema Badru na kuongeza:

“Kwa mwaka 2019/2020, Serikali imeongeza bajeti ya fedha mikopo kutoka TZS 427.5 bilioni hadi TZS 450 bilioni zinazotarajia kuwanufaisha jumla ya wanufaika 125,000 wakiwemo wa mwaka wa kwanza zaidi ya 45,000. Mwaka huu wa masomo unaomalizika ambao TZS 427.5 bilioni zimewanufaisha jumla ya wanafunzi 123,285 wakiwemo 41,345 wa mwaka wa  kwanza,” amesema Badru. 

Kambi hizo ni Bulombora, Kanembwa na Mtabila zilizopo mkoani Kigoma; Rwamkoma (Mara); Msange (Tabora); Nachingwea (Lindi); Mpwapwa na Makutupora (Dodoma); Mgambo na Maramba (Tanga). Nyingine ni Makuyuni (Arusha); Mafinga (Iringa); Mlale (Ruvuma); Itaka na Luwa (Songwe); na Milundikwa iliyopo mkoani Rukwa.  

Badru aliongeza kuwa uzoefu wa miaka iliyopita umeifanya HESLB kuandaa programu hizo ambazo alisema zimeonesha mafanikio makubwa kutokana na aina ya maswali yanayoulizwa.

“Tunawaeleza kuhusu nyaraka muhimu zinazotakiwa kuambatishwa, namna sahihi ya kuomba kwa kutumia mtandao wetu ambao upo wazi hadi Agosti 15 na tunaruhusu maswali kutoka kwao na kuyajibu papo hapo,” ameongeza.

Akizungumza baada ya mkutano huo, mwanafunzi Ngatowana Ndakwila Kiwanga ameishukuru Serikali na HESLB kwa kuandaa utaratibu wa kutembelea kambi za JKT na kuwaelimisha wanafunzi ili wawasilishe maombi kwa usahihi na hatimaye kutimiza ndoto zao za elimu.

“Mimi nimepata daraja la kwanza la pointi saba na nilikua nasoma HKL (Historia, Kiswahili na Kiingereza) na ingawa sijaomba hadi sasa, nitaomba na ninaamini nitapata mkopo na nitakua mwanasheria,” amesema Kiwanga, mwanafunzi mwenye ulemavu aliyemaliza kidato cha sita mwaka huu katika Shule ya Sekondari ya Benjamin Mkapa.

Kwa upande wake, akiongea katika mkutano huo, Mkurugenzi wa Utoaji Mikopo wa HESLB Dkt. Veronika Nyahende amesema matarajio ya HESLB kwa mwaka huu ni kuona idadi ya wanafunzi wanaokosea kujaza fomu za maombi inapungua kwa kiasi kikubwa.

“Pamoja na elimu ya maelezo ya mdomo, tumewapa kitabu kidogo cha lugha ya kiswahili chenye maswali na majibu kuhusu utaratibu mzima wa uombaji mikopo kwa lugha nyepesi…tunawasihi wasome na kuzingatia maelezo yote muhimu,” amesema Dkt. Nyahende.

Naye Mkuu wa Kikosi cha Jeshi hicho ambapo kambi hiyo yenye vijana takribani 3,000 wapo, Luteni Kanali Alex Malenda alishukuru utaratibu ulioandaliwa na kuongeza unastahili kupongezwa kwa kuwa utasaidia kupunguza muda unaotumika na wanafunzi kukamilisha maombi kwa kuwa wanakua hawajui mambo mengi.

HESLB ilianza kupokea maombi ya mkopo kwa njia ya mtandao tarehe 1 mwezi huu wa Julai na inatarajia kufunga tarehe 15 Agosti mwaka huu ili kuruhusu kazi ya uchambuzi wa maombi yaliyopokelewa na hatimaye kutoa mikopo kwa wanafunzi wenye sifa ifikapo mwishoni mwa Oktoba mwaka huu.
 Mkurugenzi wa Upangaji Mikopo wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) Dkt. Veronica Nyahende akizungumza na wanafunzi waliohitimu kidato cha sita walioko katika mafunzo ya JKT  Ruvu namna ya kuomba mkopo katika Bodi hiyo kwa ajili ya elimu ya Juu.
Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) Abdul-Razaq Badru akitoa Vitabu vya elimu kuhusu uombaji mikopo, ni Luteni Kanali Alex Malenda Katika Kambi ya JKT Ruvu kwa ajili ya Wanafunzi waliohitimu kidato cha sita walioko katika mafunzo katika Kambi hiyo.