Siku tatu baada ya kufanyika kwa sherehe ya siku ya kuzaliwa na tangazo lake rasmi kwamba mpenzi wake kutoka Kenya Tanasha Donna alikuwa ni mjamzito wa mtoto wake wa nne, nyota wa muziki wa Bongo Fleva Diamond Platinumz amechaguliwa balozi wa kukabiliana na maambukizi ya maradhi ya ukimwi TacAids.

Kulingana na Mtandao wa The Citizen nchini Tanzania Tume ya kukabiliana na janga la ukimwi nchini humo TACAIDS ilitangaza kuhusu uamuzi huo siku ya Jumatano mwezi Julai wakati wa mkutano wa tume hiyo na msanii huyo wa Wasafi Records .

Kwa mujibu wa The Citizen Tanzania kaimu mkurugenzi wa Tume hiyo Jummanne Issango alisema wakati wa mkakati wa nne wa kuangamiza Ukimwi kwamba tume hiyo inawahamasisha vijana kuhusu afya ya uzazi pamoja na kutoa hamasa kuhusu ugonjwa huo.

Akizungumza baada ya uteuzi wake Diamond Platinumz alisema kwamba iwapo wanawake wangekataa katakata kuwaruhusu wanaume kushiriki tendo la ngono bila kinga basi hatua hiyo ingepunguza maambukizi ya ugonjwa wa ukimwi nchini humo.

Kulingana na mtandao huo, Diamond alikuwa akijibu swali kutoka kwa mwandishi aliyetaka kujua ni vipi msanii huyo atafanya kampeni hiyo kupitia tamasha linalokuja la Wasafi na jinsi yeye mwenyewe alivyomwaminifu kwa wapenzi wake.

''Ninaamini kwamba iwapo wanawake watatilia mkazo swala la hakuna ngono bila kinga wanaume watalazimika kutumia kinga''.

Akizungumzia kuhusu ushirikiano wa kufanya kazi na TACAIDS kupitia tamasha la Wasafi, alisema kuwa kampeni hiyo imejiri wakati mzuri kwa kuwa tamasha hilo sio tu kuhusu burudani bali pia kutoa elimu kwa vijana.

Afisa wa baraza la sanaa nchini Tanzania Basata aliunga mkono hatua hiyo ya TACAIDS akisema kuwa walifanya uamuzi mzuri kuwatumia wasanii kutokana na ushawishi walio nao miongoni mwa Vijana kupitia mitandao ya kijamii.

Tamasha hilo la Wasafi linatarajiwa kuanza Julai 19 2019.