Msanii wa Bongo fleva Rajab Kahali maarufu Harmonize ametangaza nia ya kumsaidia msanii mwenzie Aboubakary Katwila maarufu Q Chilla ili kumrudisha tena kwenye soko la muziki baada ya kupotea.

Harmonize amesema kwa kuanzia watatoa EP (albam fupi) yenye nyimbo tatu na video zake ambazo wameshirikiana kwa pamoja na wameipa jina la ‘Return of Q Chilla’ na itaachiwa  Julai 22.

Akizungumza na waandishi wa habari, Harmonize amesema anamsaidia Q Chilla kwa kushirikiana na uongozi wa lebo ya WCB chini ya msanii Nasib Abdul maarufu Diamond Platnumz.

“Q Chilla ni msanii mkubwa hapa nchini na ndiyo chanzo cha maendeleo ya muziki wetu kwa kushirikina na uongozi wa Wasafi tumeona tushirikane na watanzania kuhakikisha kipaji chake hakipotei ili pia apate maisha mazuri na familia yake,” amesema Harmonize.