DC Afunguka Wanafunzi Kufanya Mapenzi ya Kinyume
Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Severine Lalika, ameeleza kuwa anafuatilia madai ya wanafunzi wa kike wilayani humo, kujihusisha na mapenzi ya kinyume na maumbile ili kukwepa mimba kama ambayo ilielezwa na Mkurugenzi wa Asasi ya Usaidizi wa Kisheria ya Wilaya ya Ilemela (ILABU) Mateko Jackson.

Severine Lalika, ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na EATV/EARadio Digital kwa njia ya simu,  ambapo ameeleza kwa sasa yuko mapumziko jijini Dar es salaam, hivyo anaomba muda wa kutosha ili afuatilie suala hilo.

Amesema kuwa "kwa sasa nipo mapumzikoni Dar es salaam sijaingia ofisini ila nitafuatilia suala hilo, kwa sasa naomba nikupe namba ya Afisa Elimu Msingi au Sekondari ili akueleze kuhusiana na  hayo madai".

EATV/EARadio Digital imemtafuta Afisa Elimu Msingi Ilemela Deo Msingi Musungu juu ya taarifa hizo, ameeleza na yeye yupo njiani anarudi ofisini, na hata alipoulizwa kuhusiana na mtu anayekaimu majukumu yake, amesema suala hilo inabidi alitolee ufafanuzi yeye mwenyewe baada ya kufika ofisini.

"Mimi ni kweli Afisa Elimu Msingi, lakini hizo taarifa unazonipa mi mpya kwangu, narudi ofisini leo nilikuwa safarini kwa hiyo nitafute Jumatatu nitakujibu" amesema Deo Msingi Musungu.

Hivi karibuni kupitia Mkurugenzi wa Asasi ya Usaidizi wa Kisheria ya Wilaya ya Ilemela (ILABU) Mateko Jackson, alitoa taarifa juu ya uwepo wa baadhi ya wanafunzi wa kike katika Shule za Msingi na Sekondari jijini Mwanza, wanaojihusisha na mapenzi ya kinyume na maumbile, kwa kile kilichoelezwa ni kukwepa kupata mimba na kupelekea kufukuzwa shule.