Mkurugenzi wa kitengo cha Sheria DAWASA Bi. Florence Yamati akielezea sheria mpya ya huduma ya majisafi pamoja na usafi wa mazingira kwa waandishi wa habari katika banda la DAWASA lililopo kwenye viwanja vya maonyesho ya 43  kimataifa ya Sabasaba yanayoendelea.
Mkurugenzi wa kitengo cha Sheria DAWASA Bi. Florence (wa kwanza kushoto) na Meneja Uhusiano wa Jamii wa Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dar es Salaam (DAWASA) Bi. Neli Msuya wakimsikiliza mteja katika banda lao lililopo katika Maonesho ya 43 ya Biashara ya Kimataifa ya Sabasaba yanayofanyika jijini Dar es Salaam.
Afisa Ubora Maji wa DAWASA Sizya Mongela akitoa elimu ya ubora wa maji kwa Mteja waliotembelea kwenye Banda lao kwenye Maonesho ya 43 ya Biashara ya Kimataifa jijini Dar es Salaam.
Muonekano wa Banda la DAWASA katika Maonesho ya 43 ya Biashara ya Kimataifa.


Mkurugenzi Huduma kwa Wateja wa DAWASA Ritamary Lwabulinda akizungumza na wanahabari kuwaomba wananchi kujitokeza ili waweze kuwatatulia kero zao ikiwemo kulipia ankara zao za maji. Kulia ni Mkurugenzi wa kitengo cha Sheria wa DAWASA Bi. Florence Yamati. 
Dawati la huduma kwa wateja wakiendelea kutoa huduma kwa wateja waliofika kwenye Banda la Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es salaam (DAWASA) kwenye Banda lao la Maonesho ya 43 ya Biashara ya Kimataifa jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa kitengo cha Sheria DAWASA Bi. Florence Yamati akifafanua jambo kwa mwanahabari.
Mkurugenzi Huduma kwa Wateja wa DAWASA Ritamary Lwabulinda (kushoto) akifafanua jambo kwa mmoja ya wafanyakazi wa mamlaka hiyo.
Na Cathbert Kajuna - Kajunason/MMG.

Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Mkoa wa Dar es Salaam (DAWASA) imesema itaendelea kutoa elimu kwa wananchi ili waweze kuitambua sheria mpya namba 5 ya usimamizi wa mazingira ya mwaka 2019 badala ya kufutwa sheria namba 5 ya mwaka 2001.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Sheria wa DAWASA Florence Yamati kwenye banda la Mamlaka hiyo kwenye maonesho ua 43 ya biashara ya Kimataifa yanayoendelea kwenye Viwanja vya Mwalimu Nyerere barabara ya Kilwa Jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari, Yamati amesema sheria hiyo mpya ya mwaka 2019 imebadilisha Mamlaka ya Majisafi na Majitaka na kuwa Mamlaka ya majisafi na usafi wa mazingira.

Yamati amesema, sheria hiyo mpya itasimamia mazingira na itakuwa na mfumo endelevu wa kulinda vyanzo vya maji pamoja na miundo mbinu.

"Sheria hii mpya inatutaka kulinda miundo mbinu ya maji na kuongeza faini na adhabu  kutoka 500,000 hadi 50,000,000 pamoja au kifungo," amesema.

Sheria hiyo mpya iliyopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeanza kutumia Julai Mosi mwaka huu na inawataka DAWASA kusimamia usafi wa mazingira kiujumla.

Naye Mkurugenzi Huduma kwa Wateja Ritamary Lwabulinda amewaomba wateja wa DAWASA kulipa bili zao kwa wakati ili kuweza kuendelea kuboresha huduma pamoja na kujenga miradi mipya ya maji ili wananchi wengine ambao hawapo kwenye mtandao waweze kupata huduma ya maji safi na  salama.

"DAWASA tumejipanga kuendelea kuongeza miradi ya maji kupitia malipo ya ankara zenu za maji, mtu anapolipia maji kwa wakati anasaidia kuongeza kuimalisha mtandao wa upatikanaji wa maji kwa vile kwa sasa kuna miradi inaendelezwa kwa fedha za ndani," amesema.

Mbali na hilo, Ritamary amewataka wananchi kujitokeza kwenye banda lao kwa kupata maelezo zaidi na kufahamu jinsi ya kujiunga na DAWASA.