Na Chalila Kibuda,Michuzi TV
Chuo cha Kodi kimesema kuwa wahitimu wa kidato cha sita wajiunge na chuo hicho kwa  kuwa mazingira ya chuo hicho ni rafiki kwa kusomea pamoja na wigo wa kazi kwa kujiajiri kuwa mpana kutokana kuwepo kwa mahitaji katika masuala ya forodha na kodi ndani na nje ya nchi.

Akizungumza katika maonesho ya vyuo vikuu yanayofanyika katika viwanja vya mnazi mmoja jijini Dar es Salaam Afisa Mkuu wa Mawasiliano wa Chuo hicho Oliver Njunwa amesema chuo kimejipanga vyema katika udahili wa mwaka wa masomo 2019/2020.

Amesema wanatoa kozi za forodha na kodi katika maeneo mbalimbali kutokana na kuwepo kwa mahitaji ya taaluma hiyo kadri siku zinavyokwenda.

“Serikali pamoja na kampuni mbalimbali zinahitaji wataalam wa masuala ya forodha na kodi”.

Njunwa amesema katika maonesho ya vyuo vikuu wanafanya udahili moja kwa moja hivyo wanafunzi watumie fursa hiyo kutembelea na kutatua changamoto zao katika kufanya maombi ya udahili.

Aidha amesema idadi ya waombaji katika chuo hicho imezidi kuongezeka kutokana na wananchi kukifahamu Chuo cha Kodi pamoja na umuhimu wa taaluma ya kodi katika nchi yetu ambayo dira yake ya maendeleo ni kuifanya Tanzania kuwa ya uchumi wa viwanda.



Kwa mujibu wa Njunwa, maonyesho haya yamewafanya wananchi wengi  hususan wazazi na wanafunzi wengi wafahamu fursa zilizopo baada ya kuhitimu mafunzo ya forodha na kodi ambapo wanafunzi waliohitimu katika chuo hicho wanaweza kufanya kazi katika sekta mbalimbali huku wengine wakijiajiri.

Chuo kinahakikisha mwanafunzi anajengewa uelewa wa kitaaluma, uwezo wa kutenda kazi ili anapomaliza masomo aweze kufanya kazi kwa umahiri na weledi wa hali ya juu.

Pia tumejipanga  katika utoaji wa mafunzo yenye bora ili kuweza kukidhi mahitaji ya watalaam katika masuala ya kodi pamoja na forodha kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya watalaam katika sekta hiyo.

Chuo cha Kodi kimesajiliwa na Baraza la Vyuo vya Elimu ya Ufundi na kupatiwa Ithbati ya kudumu kutoa mafunzo yafuatayo ambayo ni Astashahada ya Forodha ya Afrika Mashariki -East Africa Clearing and Freight Forwarding Practicing Certificate (CFFPC),  Astashahada ya Forodha na Kodi- Techninican Basic Certificate in Customs and Tax Management (CCTM), Stashahada ya Forodha na Kodi - Diploma in Customs and Tax Management, Shahada ya Forodha na Kodi- Bachelor Degree in Customs and Tax Management- (BCTM).

Kozi nyingine ni:- Stashahada ya Uzamili ya Forodha na Kodi – Postgraduate Diploma in Tax, Shahada ya Uzamili ya Sheria na Usimamizi wa Kodi- Masters of Arts in Revenue Law and  Administration (MARLA) kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha dare salaam na Chuo Kikuu cha Muenster cha Ujerumani.

Tunawashauri wanafunzi waendelee kutuma maombi yao kabla muda wa udahili kumalizika.
 Afisa Udahili wa Chuo cha Kodi Paschal Gomba (kulia) akiwasaidia wanafanuzi kufanya udahili wanafunzi waliotembelea banda la chuo hicho katika maonesho ya 14 ya vyuo vikuu katika viwanja vya mnazi mmoja jijini Dar es Salaam wa kwanza kulia ni Edwin Matemanga afisa udahili wa chuo cha kodi.
 Afisa Udahili wa Chuo cha Kodi Paschal Gomba akitoa maelezo kwa wanafanuzi waliotembelea banda la chuo hicho katika maonesho ya 14 ya vyuo vikuu katika viwanja vya mnazi mmoja jijini Dar es Salaam
Afisa Mkuu Mawasiliano Chuo cha Kodi, Oliver Njunwa akimfafanulia mzazi aliyetembelea maonesho ya 14 ya Vyuo Vikuu yanayofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.