Maelfu ya samaki aina ya salmon nchini Canda wanatarajiwa kuokolewa kwa ndege baada ya kukwama mtoni kutokana na maporomoko ya ardhi.
Mwezi Juni, maafisa maafisa waligundua kuwa miamba iliyoshushwa na maporomoko imeziba kipande cha mto Fraser katika jimbo la British Columbia, na kuwazuia maelfu ya samaki hao kuelekea juu ya mto ambao hutaga mayai.
Vikosi vya uokozi vimepiga kambi katika eneo hilo kupanga mkakati wa namna ya kuwaokoa samaki hao kwa kuwasafirisha mpaka upande wa pili wa mto kwa kutumia helikopta.
Watunza mazingira wametoa tahadhari kuwa inabidi kila liwezekalo lifanyike ili samaki hao watage mayai ama la idadi yao itapungua na kuwa hatarini.
Haijulikani ni samaki wangapi ambao wamenasa, lakini inaaminika kuwa ni 700 tu ambao wameweza kuvuka kikwazo hicho bila ya msaada wowote.
Maporomoko ya ardhi yamezuia njia za samaki toka mezi Juni katika mto Fraser
Makabila mengi ya asili nchini Canada wanategemea samaki hao kama chakula na bidhaa muhimu kwenye sherehe zao za jadi.
Waziri wa uvuvi wa Canada, Jonathan Wilkinson, amesema serikali imekuwa ikifanya kazi usiku na mchana kuwasaidia samaki hao.
Hata hivyo bado haijatangazwa tarehe rasmi ambapo uokozi huo wa kutumia ndege utafanyika.
Namna gani samaki hao watapandishwa ndege?
Vikosi vya uokozi kwa sasa vinatengeneza bwawa la kuwazuia samaki hao.
Baada ya kuelekezwa kwenye bwawa hilo, watawekwa matanki ya lita 780-2,700 na kunyanyuliwa na helikopta kutoka eneo hilo la maporomoko.
Matanki hayo yatapuliziwa hewa ya oxygen ili kuwasaidia samaki watulie na kufika salama.