Shirikisho la Soka Afrika (CAF) limeteua Waamuzi Wanne (4) na Makamishna Wawili(2) kutoka Tanzania kusimamia mechi za Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho.

Afisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Cliford Mario Ndimbo amesema kwamba refa Elly Sasii atasimama katikati kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa kati ya Aigle Noir ya Burundi na Gor Mahia ya Kenya utakaochezwa Uwanja wa Prince Louis Rwagasore, Burundi Agosti 11, 2019.

Ndimbo amesema Sasii atasaidiwa na Mwamuzi msaidizi namba 1 Frank Komba,Mwamuzi msaidizi namba 2 Ferdinand Chacha,Mwamuzi wa Akiba Emmanuel Mwandembwa na Kamishna wa mchezo anatokea Rwanda, Gaspard Kayijuka.

Aidha Mtanzania Ahmed Mgoyi atakua Kamishna wa mchezo wa marudiano Ligi ya Mabingwa Gor Mahia dhidi ya Aigle Noir utakaochezwa kati ya Agosti 23,24 na 25 nchini Kenya.

Naye Mtanzania Khalid Abdallah ameteuliwa kuwa Kamishna wa mchezo wa Kombe la Shirikisho kati ya Proline FC ya Uganda na Master Security Services ya Malawi utakaochezwa Uwanja wa Kampala Startimes nchini Uganda.