Mwimbaji maarufu nchini Marekani Beyonce ameachia kibao kipya hii leo, na maneno ya kwanza kabisa ni ya Kiswahili



“Uishi kwa muda mrefu mfalme,” sauti nyembamba inaimba kisha sauti nzito inaitika “uishi kwa”, kionjo hiko kinajirudia mara mbili na kisha wimbo kuendelea kwa Kingereza.

Kibao hicho kiitwacho Spirit ni sehemu ya albamu inayosindikiza filamu mpya ya Lion King inayotengenezwa na kampuni kubwa ya Disney ya nchini Marekani.

Mfalme anayeimbwa kwenye kibao hicho ni Simba dume kijana ambaye anaanza safari ya kupambana ili kuwa mfalme wa nyika.

Filamu ya Lion King, “inajumuisha sauti za kutoka barani Afrika,” imeeleza kampuni ya Disney.

Ruka ujumbe wa Youtube wa Polar Records

Onyo: Imetoka kwingine na inaweza kuwa na matangazo
Mwisho wa ujumbe wa Youtube wa Polar Records

Kampuni hiyo inasema kuwa albamu hiyo iitwayo The Lion King: The Gift, itaachiliwa ndani ya kipindi cha siku tisa kuendana na uzinduzi wa filamu hiyo duniani kote.

Albamu hiyo imejumuisha vionjo vya waandaa muziki kutoka Afrika, kwa mujibu wa Beyonce ambaye amenukuliwa kwenye taarifa iliyotolewa na Disney.

“Ilikuwa ni muhimu kuwa muziki usiimbwe na wasanii nyota na wenye vipaji bali iandaliwe na waandaaji wa Kiafrika. Ubora na moyo (mapenzi) vilikuwa vitu muhimu kwangu…

“Ni mchanganyiko wa kila kitu, si sauti moja tu. Kuna ushawishi kutoka kila kona, kutoka kwenye R&B, hip-hop na Afro Beat.”