Mahakama ya Mwanzo ya Mwandiga mkoani Kigoma, imemkuta na kesi ya kujibu Diwani wa Kata ya Mwanga Revocatus Kipando (Baba Levo), baada ya kutuhumiwa kufanya shambulio kwa Askari wa usalama barabarani akiwa kazini Julai 15, 2019.


Uamuzi huo umekuja baada Hakimu wa Mahakama hiyo Frolence Ikorongo, kusikiliza upande wa mshitaki akiwa na mashahidi wawili ambao ni Mussa Lukomati na Karume Rashidi, ambao walieleza tukio hilo lilitokea Julai 15, majira ya saa 1 usiku.

Mashahidi wameeleza kuwa Baba Levo alimshambulia askari anayefahamika kwa jina la Msafiri Ponera, akiwa eneo lake la kazi eneo la Kwabela, na inadaiwa mtuhumiwa alilazimisha kupita kwa pikipiki wakati askari huyo akiwa waruhusu watembea kwa miguu, na baada ya hapo Baba Levo aliamua kumshambulia askari huyo.

Hakimu Ikorongo amesema kuwa, "kifungu cha 240 sura ya 16 kanuni ya adhabu chapisho la mwaka 2002, Mahakama imemkuta mshtakiwa Baba Levo na kesi ya kujibu baada ya kujiridhisha na ushahidi wa mshitaki"

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Julai 30, 2019, ambapo kwa sasa mtuhumiwa Baba levo yuko nje kwa dhamana.