BAADA ya mwanamama ambaye pia ni mjasiriamali, Zarinah Hassan ‘Zari The Bosslady’ kubana kwa muda mrefu hatimaye ameachia kwa kumruhusu staa wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ kuonana na watoto wake.  Diamond anayetamba na Wimbo wa Kanyaga, alionekana kwa mara ya kwanza akitumia video call kuwasiliana na watoto wake hao wawili, Nillan na Tiffah ambao wanaishi na mama yao, nchini Afrika Kusini ‘Sauz’.

Kwa mujibu wa watu wa karibu na Diamond, alipewa ruhusa hiyo ikiwa ni siku moja baada ya kupata baraka ya kumchukua mtoto wake mwingine, Daylan aliyezaa na mwanamitindo, Hamisa Mobeto. “Ujue kwa muda mrefu Zari alikuwa hataki kabisa Diamond awasogelee watoto wake. Kama mnakumbuka kuna kipindi alisema anaweza kuwahudumia kwa kila kitu kwa hiyo hana shida naye.

“Kingine hata katika siku ya wababa duniani, Zari alijitakia mwenyewe wala Diamond hakuhusika na hiyo yote ilisababisha baada ya kutoka na Tanasha yule raia wa Kenya,” kilisema chanzo. Inaelezwa kuwa, baada ya Diamond kuwasiliana na watoto wake hao kwa mara ya kwanza, alielekea moja kwa moja kwenye sherehe ya kuzaliwa mtoto wa Mkuu wa Mkoa wa Dar, Paul Makonda, Keegan akiwa amembeba Daylan mwanzo mwisho.

Diamond na Zari walishawahi kuwa katika uhusiano wa kimapenzi ambapo walikuwa wakiishi pamoja jijini Dar na kufanikiwa kupata watoto wawili. Waliachana Februari, mwaka jana na tangu hapo wawili hao wamekuwa wakipeana vijembe mitandaoni huku Zari akimuwekea ngumu Diamond kuona watoto.