Kocha Mkuu wa Simba Mbelgiji Patrick Aussems,  amezungumzia usajili uliofanywa na klabu hiyo kuelekea msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania bara pamoja na michuano ya Kimataifa.

Aussems amesema kuwa kabla hajakwenda likizo aliacha orodha ya wachezaji nane, ambao mpaka sasa wamesajiliwa wachache kati ya hao huku akionekana kuridhishwa na viwango vya wachezaji waliosajiliwa.

Amesema, “nimefanikiwa kwa kiasi fulani mpaka sasa kuwaandaa vijana na nimeona wote wapo vizuri na wanajuhudi kubwa uwanjani. Natengeneza kikosi bora kwa ajili ya msimu ujao''.

“Niliacha majina nane kabla sijaondoka kwenda likizo, baadhi wamesajiliwa akiwemo Msudan ambaye nilimuona muda mrefu na nimempenda kiukweli ila wengine bado hawajasajiliwa lakini waliopo ni wazuri sana na wanafanya kazi kwa juhudi,” amesema Aussems.

Kwa mujibu wa Simba, mpaka sasa imebakiza nafasi ya mchezaji mmoja pekee kumsajili, baada ya kukamilisha usajili wa wachezaji wapya akiwemo, Wilker Henrique da Silva, Gerson Fraga Viera, Tairone da Silva hawa ni raia wa Brazili ambao wamesaini kandarasi ya miaka miwili.

Wengine ni Sharaf Eldin Shiboub Ali Abdalrahman raia wa Sudan, Beno Kakolanya, Miraj Athuman, Francis Kahata, Ibrahim Ajib na Gadiel Michael.