Muigizaji wa Filamu hapa nchini Steven Mengele maarufu kama Steve Nyerere, ameona fahari kufananishwa na Sanamu ya Nyerere, aliyokabidhiwa Rais Magufuli wakati wa uzinduzi wa Hifadhi ya Taifa ya Burigi Julai 9, 2019, Chato Mkoani Geita.

Akizungumza na EATV&EARadio Digital, Steve Nyerere amesema, anaona fahari na kufarijika sana kuona watanzania wanautambua mchango wake katika jamii na kudai hizo ni changamoto ambazo ni za kuzoea.

''Kwangu ni fahari, kumbe watanzania wanajua ninachokifanya kiasi cha kuweza kunifananisha na sanamu aliyokabidhiwa Rais Magufuli''.

Aidha Steve ameongeza kuwa, yeye atasimama kama kioo cha jamii na  mtu mkubwa, na kwamba ataendelea kumuenzi, Hayati Baba wa Taifa Mwl Julius Nyerere.

''Nimefarijika sana na nimeona, hata zile meseji ninazofikisha kupitia mwalimu, kuelimisha jamii, kuhakikisha watu wanamuenzi mwalimu, kwa sababu ndio Baba wa Taifa, lazima akumbukwe, kuna vizazi vinakua havimtambui mwalimu, Dunia inabadilika kila siku na kuwasahau wale walengwa waliokuwa mstari wa mbele kutuletea uhuru na kujenga Taifa.

Steve Nyerere ameendelea kusisitiza kwamba, ataendelea kumuenzi Baba wa Taifa kwa Vitendo.