Aliekuwa nahodha wa klabu ya Yanga, Ibrahim Ajib ameacha ujumbe wa mwisho kwa mashabiki pamoja na uongozi wa klabu hiyo, aliyodumu nayo kwa misimu miwili.


Hiyo imekuja siku moja baada ya kutangazwa kujiunga na mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania bara TPL, Simba SC kwa mkataba wa miaka miwili, klabu ambayo ndiyo iliyomtambulisha katika soka.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Ajib ameandika ujumbe akisema, "hakika ilikua miaka miwili bora sana kwangu, ndani na nje ya uwanja, Yanga ilikua sehemu ya familia yangu. Nitoe shukrani zangu za dhati kwa viongozi, benchi la ufundi, wachezaji na mashabiki wote kwa kuniamini na kuniunga mkono kwa kila jambo. Ni mengi nimejifunza na nina amini yatanisaidia kunijenga zaidi kama mchezaji. Asanteni sana."

Ajibu alicheza kwa kiwango kikubwa msimu uliopita akiwa na Yanga, ambapo alifanikiwa kuibuka mtoa 'assist' bora wa TPL, akitoa jumla ya 'assist' 14 na kuisaidia Yanga kumaliza nafasi ya pili katika msimamo wa ligi.