Aishi na maiti ya mama yake kwa miaka mitatu

Mwanamke mmoja jimboni Texas, Marekani amekamatwa baada ya masalia ya maiti ya mamake inayooza kugunduliwa nyumbani wanakoishi pamoja


Polisi wanaamini mwanamke huyo mwenye umri w amiaka 71 alianguka mnamo 2016.

Wamtuhumu kwamba binti yake mwenye umri w amiaka 47 alishindwa kumhudumia vizuri mama yake aliyefariki “siku chache baadaye” kutokana na athari ya kuanguka huko.

Masalio ya mwili wa marehemu yalipatikana kwenye sakafu ya chumba kimoja. Binti yake na mjukuu wake marehemu walilala katika chumba cha pili katika nyumba hiyo.

Kwa mujibu wa shirika la habari la BBC,  Mjukuu wa marehemu alikuwa na miaka 15 wakati akiishi na maiti ya bibi yake. Na kutokana na hilo, mamake ameshtakiwa kwa ‘kumdhuru mtoto’ wa chini ya miaka 15.

Mjukuu huyo sasa anatazamwa na jamaa zao na anapokea usaidizi kutoka kitengo cha kuwalinda watoto.

Huenda mamake akakabiliwa na hadi miaka 20 gerezani na faini ya hadi $10,000.

Polisi wanasema marehemu bibi huyo aliheshimika katika jamii kwenye eneo hilo, na alifanya kazi kama karani na mwalimu msaidizi katika mojawapo wa shule katika eneo hilo kwa miaka 35.

Alipostaafu, alikuwa akifanya kazi ya kukusanya tiketi katika sherehe za michezo huko Seguin.