Afisa wa zamani wa shirika la umoja wa mataifa amefungwa jela nchini Nepal baada ya kukutwa na hatia ya udhalilishaji wa watoto.

Peter John Dalglish, 62 raia wa Canada, alishikiliwa karibu na mji wa Kathmandu mwaka 2018 na kuhukumiwa mwezi uliopita.

Alihukumiwa kifungo cha miaka tisa kwa kumdhalilisha mtoto wa kiume wa miaka 12 na kifungo cha miaka saba kwa kumdhalilisha kingono mtoto wa miaka 14.

Dalglish, afisa wa juu wa masuala ya kibinaadamu tangu miaka 1980, alikana mashtaka na wanasheria wake waliliambia shirika la habari la Reuters kuwa wangekata rufaa.

Dalglish pia aliamriwa kulipa fidia kiasi cha pauni 3,600 kwa kila mtoto. Watoto hao walikuwa nyumbani mwa afisa huyo alipokamatwa.

''Jaji hajaamua kama Dalglish atatumikia kifungo cha miaka 16 kwa ujumla au aachiwe baada ya miaka tisa''.

''Katika kesi za namna hiyo , hukumu hutumikiwa kwa pamoja lakini ni juu ya jaji kuamua'' Afisa wa mahakama aliliambia shirika la habari la Ufaransa, AFP.

Dalglish alikuwa afisa wa masuala ya kibinaadamu aliyeheshimika sana, akijihusisha na miradi mbalimbali duniani.

Mwaka 2016, alipatiwa tuzo iliyotambua mchango wake kwa watoto walio kwenye mazingira magumu.

Alikuwa sehemu ya uanzishwaji wa taasisi inayowasaidia watoto wa mitaani miaka ya 1980, Street Kids International, ambayo baadae iliunganishwa na Save the Children.

Dalglish alishika nafasi za juu za mashirika ya UN, ikiwemo shirika linaloshughulikia makazi la umoja wa mataifa nchini Afghanistan mwaka 2015.

Nchini Nepal, Dalglish alikuwa mshauri wa shirika la kazi duniani mwanzoni mwa miaka ya 2000.