Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni kubwa zaidi ya mawasialiano ya simu Afrika Mashariki Safaricom, Bob Collymore ameaga dunia, kampuni hiyo imethibitisha.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Safaricom, Collymore amefikwa na umauli asubuhi ya leo Jumatatu Juni Mosi 2019 nyumbani kwake jijini Nairobi.

Mwenyekiti wa kampuni hiyo Nicholas Ng'ang'a amesema kuwa afya ya Collymore ilikuwa mbaya majuma ya hivi karibuni.

Collymore, alichukua likizo ya matibabu ya miezi tisa mwishoni mwa mwaka 2017 na kuelekea nchini Uingereza kwa ajili ya matibabu ya saratani .Alirejea Kenya mwezi Juni mwaka jana. Gazeti la Standard media nchini Kenya limeripoti.

Marehemu ameacha mke na watoto wanne.

Collymore alianza kuongoza gurudumu la Safaricom mwaka 2010 kutoka kwa Michael Joseph ambaye kwa sasa ni mmoja wa wajumbe wa bodi ya kampuni hiyo, pia mwenyekiti wa bodi ya shirika la ndege la Kenya Airways.

Mwaka 2017 wanahisa walipiga kura kuongeza mkataba wa Bob Collymore kwa miaka miwili baada ya mkataba wake kuisha. Mkataba aliokuwa akiufanyia kazi ulikuwa unatarajiwa kufikia tamati mwaka 2020 na kumfanya kuwa Mkurugenzi aliyekalia kiti hicho kwa muda mrefu zaidi kwenye historia ya kampuni hiyo.