Na Mathew Kwembe, Chemba, Dodoma
Aliyewahi kuwa Afisa Elimu Sekondari wa Wilaya ya Chemba  iliyopo mkoani Dodoma Mwalimu David Mwamalasa ambaye hivi sasa amehamishiwa wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma amesimamishwa kazi na serikali kwa muda wa wiki mbili ili kupisha uchunguzi dhidi yake wa matumizi mabaya ya fedha kiasi cha shilingi milioni 259 ambazo zililetwa na serikali kupitia Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa ajili mradi wa P4R kwenye Shule za sekondari za Mondo na Soya  zilizopo wilayani Chemba, katika mkoa wa Dodoma.

Agizo la kumsimamisha Afisa Elimu huyo limetolewa na Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe.Mwita Mwikwabe Waitara (MB) mara baada ya kufanyika mkutano wa hadhara shuleni hapo ambao uliwahusisha wanafunzi, walimu na wakazi wa kijiji cha Mondo, katika wilaya ya Chemba.

Sambamba na kusimamishwa kwa Afisa elimu huyo ambaye alihamishiwa wilayani Chamwino mkoani Dodoma, Mhe.Waitara amemwagiza Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhandisi Joseph Nyamuhanga kuunda timu ya uchunguzi itakayokwenda shuleni hapo ili kuchunguza tuhuma hizo.

“Timu ije hapa ndani ya wiki mbili tupate fedha zilizoelekezwa kwa nini zimetumika kinyume na maelekezo, hayo ndiyo maelekezo yangu,” amesema Mhe.Waitara na kuongeza:

“Jambo lingine ambalo nimemwelekeza Katibu Mkuu, ni la kuhakikisha kuwa kuanzia sasa mtumishi anapofanya makosa eneo moja asihamishwe kwenda eneo linguine kwa nafasi yake ileile na kwa kweli hatupendelei kama viongozi, hata Mhe.Rais hataki, mtendaji yoyote ambaye atakuwa TAMISEMI amefanya makosa katika shule ya Mondo, natolea mfano kwa nafasi hiyo hiyo, hatuwezi tukawa tunasambaza uozo, kama mtu amekosa achukuliwe hatua, kama ni kuwa demoted (kushushwa cheo) ama kufukuzwa kazi ili na wengine wajifunze wasifanye makosa yale yale.”

Naibu Waziri amesema serikali haiwezi kuendelea kuwa na mtindo wa aina hiyo ambapo unafanya makosa sehemu A unahamishiwa sehemu B, badala yake akataka mhusika anapokutwa na makosa awajibishwe kwa kuondolewa nafasi yake ili apishe watumishi wengine ili wachukue nafasi hiyo.

Pia Mhe.Waitara alitumia mkutano huo kueleza bayana kuwa serikali haina mpango wa kufuta ngazi za kidato cha tano na sita katika shule hiyo na badala yake itaelekeza nguvu zake katika kuiboresha shule hiyo kwa kuiongezea miundombinu ya shule na walimu shule hiyo ili iweze kufanya vizuri katika mitihani itakayofanyika siku za usoni.

Amesema kuwa kamwe hatarajii kuona shule hiyo ikiondoa michepuo ya kidato cha tano kwani shule hiyo ina michepuo mitatu ya sayansi shuleni hapo na ni jukumu la serikali kuhakikisha kuwa miundombinu hiyo inaboreshwa kadri siku zinavyosonga mbele.

Awali Mratibu wa Mradi wa P4R (Lipa kwa matokeo) kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI Bi Mary Machaku alimweleza Naibu Waziri kuwa shule ya Mondo ilikuwa ni miongoni mwa shule 86 ambazo zilikuwa kwenye mpango wa serikali wa kuanzisha kidato cha tano.

Amesema kiasi cha shilingi milioni 259 zilizoletwa katika shule za Mondo na Soya wilayani Chemba zilileletwa na maelekezo mahsusi ambapo Afisa Elimu Sekondari wa wilaya pamoja na Mkuu wa shule walipaswa kuwatolea nakala wajumbe wa Bodi ya shule ili watekeleze maagizo ya namna ya kuzitumia fedha hizo na siyo kubadilisha matumizi kwa kuziachia bodi za shule  kutengua maelekezo ya Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI.

Amesema kwa mujibu wa maelekezo ya TAMISEMI, fedha hizo zilipaswa kujenga mabweni mawili yenye kubeba wanafunzi 80 wa kidato cha tano kwa kila bweni, pia ujenzi wa vyumba vinne vya madarasa kwa gharama ya shilingi milioni 20 kwa chumba kimoja cha darasa, hivyo jumla milioni 80 kwa vyumba vinne.

“Pia tulileta milioni 11 na laki moja kwa ajili ya ujenzi wa matundu 11 ya vyoo, sambamba na hilo tuliwaletea shilingi milioni 18 kwa ajili ya ukarabati wa maabara moja ambayo itakapokamilika iwe na mifumo ya maji, umeme na samani zake za ndani, ambapo total yake inaleta shilingi milioni 259,” amesema.

Katika utetezi wake, afisa elimu Mwamalasa alisema kuwa  maelekezo yote ya TAMISEMI kuhusu matumizi ya fedha hizo yalitekelezwa isipokuwa kwenye eneo la ujenzi wa vyumba vinne vya madarasa ambapo bodi ya shule iliona afadhali ikarabati vyumba vitatu vya madarasa katika shule hiyo ambavyo vilikuwa vimeharibika kabisa, na vyumba vitatu vingine ambavyo vilirudiwa kufanyiwa kazi.

Mwamalasa amesema kuwa fedha hizo pia zilitumika kununulia vitanda 160, ukarabati wa ukumbi wa kulia chakula, na kuweka uzio upande wa mbele na nyuma kwa ajili ya kuimarisha usalama wa wanafunzi wa kike katika shule hiyo.

Mkutano huo pia ulihudhuriwa na Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Chemba ambaye pia ni Mkuu wa wilaya ya Kondoa Mh. Sezaria Makota, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chemba Dkt.Semistatus Mashimba, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Uratibu wa Elimu kutoka TAMISEMI Bibi Odilia Mushi.
 Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe.Mwita Mwikwabe Waitara (MB)  akimwangalia mwanafunzi Faidha Rashid ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha tatu jinsi anavyojibu swali la hesabu shuleni hapo. 
 Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe.Mwita Mwikwabe Waitara (MB) akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Mondo.
Kaimu Mkuu wa wilaya ya Chemba ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Kondoa Mh. Sezaria Makota akiwa na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya uratibu wa elimu Bibi Odilia Mushi.