Ili kuhakikisha kuwa kazi ya usambazaji umeme mijini na vijijini inafanyika kwa kasi na ufanisi katika mwaka wa fedha 2019/20, viongozi wa Wizara ya Nishati wakiongozwa na Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani wamefanya Mkutano wa siku moja na watendaji wa TANESCO na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ili kujadili masuala mbalimbali yatakayowezesha lengo hilo linafanikiwa.
Mkutano huo, uliofanyika tarehe 16 Juni, 2019, ulihudhuriwa na Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati, Dkt. Hamisi Mwinyimvua, Menejimenti ya TANESCO, REA na Bodi ya REA, ulijadili kazi zilizofanyika katika mwaka 2018/19 na kujipanga katika utekelezaji wa majukumu kwa mwaka wa fedha wa 2019/20 unaoanza mwezi Julai.
Baadhi ya masuala yaliyojadiliwa kwenye kikao hicho ni upelekaji umeme viwandani, kuimarisha hali ya umeme katika maeneo yaliyounganishwa na gridi, kuunganishia umeme Taasisi za umma, kuunganishia umeme maeneo yaliyopitiwa na miundombinu ya umeme, bei ya kupeleka umeme vijijini, ununuzi vifaa vya umeme, utambuzi wa wateja wanaohitaji umeme viwandani na utambuzi wa wazalishaji wadogo wa umeme.
“ Kimsingi lazima tuhakikishe tunaimarisha huduma za umeme kwa kutatua kero mbalimbali kama za kukatika kwa umeme na kutowaunganishia umeme wateja ndani ya muda uliopangwa hivyo lazima tujipange sasa kukamilisha shughuli zetu kwa ukamilifu ili kuwezesha nchi kuingia kwenye uchumi wa viwanda.” Alisema Dkt Kalemani
Suala la upelekaji umeme viwandani, Waziri wa Nishati, amesema kuwa ni la kipaumbele na ametoa miezi mitatu kwa Mameneja wa TANESCO wa Wilaya kuwasilisha takwimu ya viwanda walivyoviunganishia umeme kwenye maeneo yao.
Aidha, amewaagiza kuhakikisha kuwa, wanafanya jitihada za kuunganishia umeme viwanda vinavyoanzishwa kwenye maeneo yao kabla havijakamilika kwa kupeleka bili stahiki kwa wenye viwanda ili waweze kufanya malipo mapema hivyo TANESCO kutoonekana kuwa ni chanzo cha kukwamisha ufanyaji kazi wa kiwanda.
Kuhusu upelekaji umeme vijijini, Dkt Kalemani amesema kuwa kila mtumishi wa Wizara, TANESCO na REA lazima atambue kuwa, lengo la Serikali ni kupeleka umeme katika Vijiji vyote ifikapo Juni 2021 hivyo ni lazima kila mmoja ahakikishe kuwa hilo linafanikiwa na bei ya kuunganisha umeme ni 27,000 na Meneja asiyetaka kutekeleza hilo aachie ngazi.
Aidha, kuhusu Wazalishaji wadogo wa umeme ameelekeza Mameneja wa TANESCO wilayani kuhakikisha kuwa, wanawatambua wazalishaji hao, wanawapa elimu, miongozo, wanawasimamia na kuwaingiza katika programu za uzalishaji umeme.
Suala jingine lililojadiliwa ni ununuzi wa vifaa vya umeme, ambapo Dkt Kalemani amesema kuwa mtendaji anapaswa kusimamia utekelezaji wa agizo la Serikali la kutonunua nje vifaa vya umeme vinavyopatikana nchini ili kurahisisha ufuatiliaji wa vifaa hivyo pia kuokoa muda mrefu ambao ungetumika kusafirisha vifaa hivyo kutoka nje ya nchi.
Suala la uunganishaji umeme kwa wateja wa muda mrefu pia lilijadiliwa ambapo Waziri wa Nishati ametoa mwezi mmoja kwa TANESCO kuunganishia umeme wateja wote waliolipia umeme kwa muda mrefu na bado hawajaunganishwa na umeme.
Kazi ya kushusha umeme kwenye maeneo yaliyopitiwa na miundombinu ya umeme ameagiza kuwa, kazi hiyo ianze mwezi wa Saba mwaka huu na ikamilike ndani ya miezi Sita.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu amesisitiza kuhusu upelekaji umeme kwenye Taasisi za umma kama vile Shule, Zahanati na Visima vya Maji kutokana na umuhimu wake kwa jamii zinazozunguka maeneo hayo na kuagiza kuwa suala hilo liwekewe mkakati maalum.
Vilevile amempongeza Waziri wa Nishati kwa kuwa na utaratibu wa vikao kazi ambavyo vimekuwa na tija katika uendelezaji wa Sekta ya Nishati nchini.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt Hamisi Mwinyimvua amempongeza Waziri wa Nishati kwa Mkutano huo na kuahidi kuwa changamoto mbalimbali zilizojadiliwa kwenye Mkutano zitafanyiwa kazi.
Aidha, amegiza watendaji wa Taasisi zilizohudhuria Mkutano huo kutekeleza ipasavyo maagizo yaliyotolewa na Waziri wa Nishati na kuendelea kufanya kazi kwa bidii.
Kaimu Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga amemshukuru Waziri wa Nishati kwa kufanya Mkutano huo ambao unasaidia kuboresha utendaji kazi na kutoa wito kwa TANESCO kuendelea kutatua changamoto mbalimbali kama za kukatika umeme na kutounganishia umeme wateja ndani ya muda mfupi.
Watendaji kutoka Wizara ya Nishati na TANESCO wakiwa katika kikao baina ya Wizara ya Nishati, TANESCO na REA kilichofanyika jijini Dodoma na kuongozwa na Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani.
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, akizungumza wakati wakati wa kikao baina ya Wizara ya Nishati, TANESCO na REA kilichofanyika jijini Dodoma na kuongozwa na Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani.
Watendaji kutoka Wizara ya Nishati na TANESCO wakiwa katika kikao baina ya Wizara ya Nishati, TANESCO na REA kilichofanyika jijini Dodoma na kuongozwa na Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani.
Watendaji kutoka Wizara ya Nishati, Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na TANESCO wakiwa katika kikao baina ya Wizara ya Nishati, TANESCO na REA kilichofanyika jijini Dodoma na kuongozwa na Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt Hamisi Mwinyimvua akizungumza katika kikao baina ya Wizara ya Nishati, TANESCO na REA kilichofanyika jijini Dodoma na kuongozwa na Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani.
Watendaji kutoka Wizara ya Nishati, Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na TANESCO wakiwa katika kikao baina ya Wizara ya Nishati, TANESCO na REA kilichofanyika jijini Dodoma na kuongozwa na Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani.