Shirika la afya ulimwenguni WHO limeripoti kuhusu hatua za maendeleo zilizopigwa katika kupambana na magonjwa yanayoambukizwa kupitia ngono STD, na kuonya kutobweteka kutokana na ongezeko la matumizi ya mitandao ya kukutana wapenzi. Zaidi ya watu milioni moja wanaambukizwa magonjwa kupitia ngono kila siku duniani kote, ambapo magonjwa kama chlamydia, kisonono, trichomaniasis na kaswende yanaleta wasiwasi mkubwa.

Kwa wastani, takriban mtu mmoja katika kila watu 25 duniani ana aina moja ya magonjwa hayo, limesema shirika la WHO katika ripoti jana Alhamis.Teodora Wi afisa wa utabibu katika idara ya afya ya uzazi na utafiti katika shirika hilo, amesema watu wanapuuzia kuhusu kinga, na kuongeza kwamba hali hiyo inatisha katika wakati ambao ngono inapatikana kirahisi kupitia app za kukutana wapenzi.