Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Innocent Bashungwa amesema Serikali itatafuta wanunuzi wa zao la Tumbaku endapo Kamapuni iliyokuwa inanunua awali ya TLTC haitaendelea na ununuzi huo.

Amesema kuwa tayari Kampuni ya GTI imekubali kushirikiana na Serikali kununua zao hilo kutoka kwa wakulima msimu ujao.Mhe. Bashungwa ameyasema hayo leo alipokutana na wawakilishi wa Kampuni ya Sigara Tanzania (TCC) ambapo aliahidi kufanya mazungumzo na Waziri wa Kilimo kwa lengo la kujadiliana namna ya kupata kampuni itakayoweza kununua zao la tumbaku kutoka kwa wakulima.

‘’Tutazungumza na kampuni ya awali iliyokuwa ikinunua tumbaku kama watakubali kuendelea kununua zao hilo au kama hawawezi basi serikali itatafuta wanunuzi wengine watakaonunua zao hilo kwa wakulima msimu ujao,’’ alisisitiza.

Aliongeza kuwa wadau wengi wameipongeza serikali kwa kuwa na bajeti rafiki iliyosikiliza wadau wa viwanda na biashara kuhusu masuala ya tozo na kodi mbalimbali.

Bashungwa alisema Serikali itaendelea kuondoa vikwazo vilivyokuwepo kwenye sekta ya biashara kwa lengo la kuleta unafuu na kukuza biashara, ajira na mazingira rafiki kwa wafanyabiashara wa sekta binafsi.

Naye, Mkurugenzi wa Mahusiano Godson Killiza kutoka TCC alisema kitendo cha serikali kupunguza kodi ya bidhaa mbalimbali ni jambo linaloleta faida kwa wafanyabiashara watanzania kutumia malighafi za ndani kuzalisha bidhaa.

Alisema bajeti ya serikali ya 2019/2020 italeta faida katika ukuaji wa uchumi, kukuza biashara na kupunguza gharama za uzalishaji kwa kampuni nyingi.

Killiza alisema ongezeko la Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa asilimia nane katika biashara yao imesaidia kuongeza ulipaji wa kodi kutoka Sh bilioni 227 mwaka 2017 hadi Sh bilioni 234 mwaka jana.