WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametoa mwaka mmoja kwa viongozi wa mikoa ya Dar-es-salaam, Morogoro, Iringa, Njombe, Mbeya, Rukwa, Singida na Shinyanga ihakikishe iwe imekamilisha kuandaa Mwongozo wa Uwekezaji.

Pia amewataka viongozi wa mikoa na halmashauri zote nchini wahakikishe wanaanzisha vituo vya uwezeshaji wananchi kiuchumi kama kile cha Kahama ili kuharakisha nia ya Serikali katika kuwezesha wananchi kiuchumi.

Ametoa maagizo hayo leo (Jumamosi, Juni 15, 2019) wakati akifungua Kongamano la Nne la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi katika ukumbi wa Hazina jijini Dodoma. Kongamano hilo limeandaliwa na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi(NEEC) na kauli mbiu yake ni Wezesha Watanzania Kujenga Viwanda.

Hata hivyo, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuliagiza Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi kuratibu mifuko yote ya uwezeshaji wananchi kiuchumi ikiwemo ya Serikali na ile ya binafsi ili kujua ipo mingapi na inamnufaisha nani na je wanufaika wanajijua na ni kweli wananufaika na kisha wampelekee taarifa.

Waziri Mkuu amesema mikoa yote iliyokamilisha kuandaa mwongozo wa uwekezaji, nayo ifikapo mwakani inapaswa kuonesha hatua za utekelezaji katika kutumia fursa mbalimbali zilizoainishwa pamoja na mikakati ya kutangaza fursa hizo zilizopo katika maeneo yao.

Kadhalika, Waziri Mkuu amesema matokeo ya tafiti ziliyofanywa na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) kuhusu biashara na uwekezaji nchini yanatarajiwa kuchangia kwa kiasi kikubwa katika uandaaji wa maandiko ya miradi mikubwa inayopendekezwa na shirika hilo.

“Miradi hiyo ni pamoja na ule wa “Harmonized Innovation Solutions for Local Economic Development” ambao upo katika hatua za maandalizi. Lengo la UNDP ni kuhakikisha kuwa miradi inayohusu uwezeshaji wananchi kiuchumi inatekelezwa moja kwa moja na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ambalo lipo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu.”

Amesema NEEC ina uwezo mkubwa katika kusimamia miradi mbalimbali ya uwezeshaji ambayo imekuwa ikifadhiliwa na Serikali pamoja na Jumuiya ya Kimataifa ikiwemo UNDP, ILO, UNCTAD, AfDB na UN-Women, hivyo ameyahakikishia mashirika hayo kuwa Serikali itasimamia kikamilifu utekelezaji wa miradi yote ili kupata matokeo yaliyo tarajiwa.

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuziagizamamlaka zote zishirikiane na NEEC kuhakikisha kuwa fursa za uwezeshaji wananchi kiuchumi zilizobainishwa kupitia tafiti za UNDP zinafanyiwa kazi. “Aidha, hakikisheni kuwa Miradi mikubwa ya uwezeshaji wananchi kiuchumi inatokana na tafiti hizo”

Amesema anaimani kubwa kuwa kupitia utekelezaji wa miradi hiyo, malengo mbalimbali ya nchi kuhusu uwezeshaji wananchi kiuchumi yatafikiwa. Baadhi ya malengo hayo ni pamoja na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2015 - 2020; Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano; Dira ya Taifa ya Miaka 25; na Malengo Endelevu ya Maendeleo ya umoja wa Mataifa (SDGs).

Pia Waziri Mkuu amelitaka Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi liendeleekuratibu masuala ya uwezeshaji wananchi kiuchumi ikiwemo utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa kipindi cha 2015 - 2020 kuhusu uanzishwaji wa viwanda vidogo, vya kati na vikubwa vya kuchakata mazao ya kilimo, mifugo, uvuvi na misitu.

“Mifuko ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi iboreshwe sambamba na kuongeza ufanisi ili iweze kuwafikia Watanzania wengi hususan wale wa vijijini. Vilevile, kamilisheni na hakikisheni mnazindua haraka mfumo wa kupima mifuko ya uwezeshaji kwa matokeo ya kiuchumi na kijamii na siyo kwa shughuli walizofanya.”

Amesema uwezeshaji wananchi kiuchumi ni suala mtambuka, sekta mbalimbali za kiuchumi na sekta binafsi zinajihusisha moja kwa moja katika kuwawezesha wananchi kiuchumi, hivyo, amesisitiza kwamba ni muhimu sana masuala ya uratibu, ufuatiliaji na tathimini ya shughuli za uwezeshaji wananchi kiuchumi, yakafanywa mara kwa mara ili kuweza kufikia malengo waliyojiwekea.
(mwisho)