Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa amesema wataendelea kuondoa urasimu katika sekta ya viwanda kwa kutumia Mpango wa Maboresho ya Mazingira ya Biashara (blue print) kwa lengo la kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji.

Aidha, amesema watafanya mazungumzo na kampuni inayonunua zao la tumbaku kwa wakulima kuona kama wataendelea kufanya hivyo au serikali itafute wanunuzi wengine walio tayari.

Akizungumza na ujumbe kutoka Umoja wa Ulaya (EU), Dar es Salaam jana, Bashungwa alisema utekelezaji wa mpango huo unahitaji ushirikiano baina ya taasisi za serikali, sekta binafsi, wadau wa maendeleo na wahisani.

Bashungwa alisema mpango huo utaleta ufanisi kuanzia kwa wazalishaji wa mazao ya kilimo na wafanyabiashara ambapo malighafi zitakazozalishwa zitakuwa na ubora unaotakiwa na zitaweza kutumika popote duniani. “Blue print itasaidia kuongeza biashara kwa masoko ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Nchi za Jangwa la Sahara (SADC) na Umoja wa Ulaya.

Utasaidia Tanzania kufikia uchumi wa wa kati,” alisema Bashungwa. Alifafanua kuwa mpango huo pia utaongeza ufanisi katika biashara na shughuli za viwanda katika kuongeza uzalishaji ambao utasaidia wafanyabiashara kulipa kodi zaidi serikalini na kujenga uchumi jumuishi kupitia ajira kwa vijana na wanawake. Aidha, alisema serikali itaendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo na sekta binafsi kwa ajili ya kuondoa vikwazo vinavyokwamisha uwekezaji ikiwemo tozo mbalimbali kama ilivyofanywa kwenye bajeti ya 2019/2020.

Naye Mkuu wa Kitengo cha Ushirikiano kutoka EU, Joseph Nunes alisema wataendelea kuisaidia serikali katika maeneo mbalimbali ya uwekezaji watakayotaka wafanye ikiwemo masoko, ajira na huduma za jamii.

Nunes alisema tozo zaidi ya 54 zilizoondolewa na serikali itachochea maendeleo katika sekta mbalimbali na kwamba mpango wa blueprint utaongeza uwajibikaji hivyo kuwa na ushirikiano wa kiuchumi utakaoleta tija. Katika hatua nyingine, waziri huyo alizungumza na wadau kutoka Kampuni ya Sigara Tanzania (TCC) na kuwaahidi kufanya mazungumzo na Waziri wa Kilimo kwa lengo la kujadiliana namna ya kupata kampuni itakayoweza kununua zao la tumbaku kutoka kwa wakulima.