Wapenzi wawili jinsia moja wanasema kuwa walishambuliwa na kuwachwa na damu katika nguo zao baada ya kukataa kupigana busu katika basi.

Melania Geymonat mwenye umri wa miaka 28 alisema kuwa shambulio hilo dhidi ya mpenzi wake Chris lilitokea katika basi moja la usiku mjini London walipokuwa wakisafiri kuelekea mji wa Camden mapema tarehe 30 mwezi Mei.

Kundi moja la vijana lilianza kuwasumbua wakati walipogundua kwamba wanawake hao ni wapenzi wakiwataka kupigana busu mbali na vitendo vya kushiriki ngono.

Kampuni ya basi ya Metroline imesema kuwa ina kanda ya CCTV kuhusu unyanyasaji huo na inashirikiana na maafisa wa polisi wa Met.

''Maafisa wanafuatilia kisa hicho katika kanda moja ya CCTV'' , alisema msemaji mmoja wa polisi.

Bi Geymonat anasema kuwa ameshawahi kukabiliana na matusi , lakini akaongezea kwamba hajawahi kupigwa kutokana na jinsia yake.


Bi Geymonat alisema: Walituzingira na kuanza kutoa maneneo machafu dhidi yetu- kama jinsi ya kushiriki ngono, wapenzi wa jinsia moja na wakatuambia tupigane busu ili watutazame.

''Ili kuondoa wasiwasi uliokuwepo kati yetu niliamua kufanya mzaha, kwamba Chris alikuwa haelewi kwa kuwa sio mzungumzaji wa Kiingereza''.

''Alijifanya kuwa mgonjwa...lakini wakaanza kuturushia sarafu na kilichofuatia ni Chris alikuwa katikati ya basi na wakaanza kumpiga''.

''Nilienda eneo hilo na nikaanza kumuokoa lakini ghafla bin vuu wakaanza kunipiga hata nami. Nilitokwa na damu nyingi''.

Maafisa wa polisi ni watu wazuri sana tunawasiliana nao na wanachunguza.

Bi Geymonat aliongezea kuwa genge hilo la watu wanne huenda lilivunja pua yake wakati wa kisa hicho na kumuiba simu na begi kabla ya kutoroka.

Wanawake wote wawili walikimbizwa hospitalini kwa matibabu kutokana na majeraha ya usoni.

Bi Geymonat alisema kuwa mmoja wao alikuwa akizungumza lugha ya kispanish huku mwengine akiwa na lahaja ya Kiingereza.

Meya wa mji wa London Sadiq Khan alisema shambulio hilo linachukiza na unyanyasaji mkubwa dhidi ya wanawake.