Wanafunzi watatu wamefariki dunia kwa ajali ya maji baada ya baada ya Mtumbwi uliokuwa umebeba wanafunzi watano wa kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Makurugusi, Wilayani Chato Mkoani Geita  kupinduka eneo la Kibumba Mwaro wa Matofari.

Kwa mjibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Mponjoli Mwabulambo, amesema ,tukio hilo limetokea majira ya saa tano asubuhi wakati wanafunzi hao, Diana Fitina(16), Asa Gabriel(19), Mayencha Faustine(18), Masalu Hamis (22) Yohana Jamonda (19) walipofika eneo hilo kwa lengo la kufanya mafunzo kwa vitendo kuhusu Mazingira ya Ziwa Victoria.

Amesema, tukio hilo limetokea umbali wa mita 120 kutoka fukwe za Ziwa Victoria,baada ya kijana Samson Kano,aliyekuwa ndani ya mtumbwi huo  mali ya Daud Thomas,kujitosa majini kwa lengo la kuwaonyesha wenzake ujuzi wa kuogelea.

Amewataja waliokufa maji kuwa ni pamoja na Asa Gabriel, mkazi wa kijiji cha Muhororo, Manyencha Faustine na Masalu Khamis, huku Diana Fitina akilazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Chato kwa matibabu, baada ya kunywa maji mengi.

Aidha,tukio kama hili limewahi kutokea Mei 22, 2017 baada ya wanafunzi watatu kati ya 24 wa shule ya msingi Butwa Kata ya Izumacheli wilayani Geita, kufariki dunia baada ya mtumbwi waliokuwa wakisafiria kutoka shuleni kuingiwa na maji na wao kujirusha majini na kuzama, huku  21 wakiokolewa.