Wabunge kesho wanatarajiwa kupiga kura kupitisha Bajeti Kuu ya Serikali ya 2019/20 ya Sh trilioni 33.11 kwa kuitwa majina na kupiga kura ya Ndiyo au Hapana.

Bajeti hiyo Kuu ya Serikali itapitishwa kama kura za Ndiyo zitakuwa nyingi zaidi ya kura za Hapana.

Ikiwa kura za Hapana zitakuwa nyingi zaidi, Bajeti Kuu ya Serikali haitapita na moja ya athari ya tukio hilo ni Rais kuwa na mamlaka ya kulivunja Bunge endapo litakwamisha Bajeti Kuu ya Serikali kupita.

Kwa kawaida upigaji wa kura, huongozwa na Spika wa Bunge, Job Ndugai, lakini kuna kila dalili upigaji kura huo kesho kuongozwa na Naibu Spika, Dk Tulia Ackson ambaye ndiye aliyeongoza mjadala wa bajeti kwa wiki nzima kutokana na Spika Ndugai kuwa nje ya nchi.

Matokeo ya kura zilizopigwa, yatatangazwa na Katibu wa Bunge, Steven Kigaigai jioni baada ya wabunge wote waliopo bungeni kupiga kura. Idadi ya wabunge waliopo bungeni, wa CCM ni 288, Chadema 62, CUF 39, NCCR Mageuzi 1 na ACT Wazalendo 1.

Kanuni za Kudumu za Bunge Toleo la Januari 2016 Kifungu cha 107 (1) kinaeleza kuwa Mjadala kuhusu Bajeti ya Serikali utakapomalizika, Spika atalihoji Bunge litoe uamuzi wake wa kupitisha au kutokupitisha bajeti ya serikali ili kukidhi matakwa ya Ibara ya 90 (2) (b) ya Katiba.

Nacho Kifungu cha 107 (2) cha Kanuni hizo, kinasema Uamuzi wa Bunge wa kupitisha au kutokupitisha Bajeti ya Serikali, utafanywa kwa kupiga kura ya wazi kwa kuita jina la mbunge mmoja mmoja Bajeti hiyo ya serikali iliwasilishwa bungeni Juni 13, mwaka huu na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango, na imejadiliwa na wabunge kwa wiki nzima tangu Jumatatu, Juni 17 hadi leo.

Akiwasilisha bajeti hiyo, Waziri Mpango alisema mapendekezo ya serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka 2019/20 ni ya Sh trilioni 33.11, kati yake Sh trilioni 20.86 sawa na asilimia 63.0 ya bajeti, ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida, zikijumuishwa Sh trilioni 9.72 kwa ajili ya ulipaji deni la serikali na Sh trilioni 7.56 kwa ajili ya mishahara.

Dk Mpango alisema Sh trilioni 3.58 zimetengwa kwa ajili ya matumizi mengineyo, zikijumuisha Sh bilioni 460.5 kwa ajili ya matumizi yatokanayo na vyanzo vya ndani vya halmashauri.

"Aidha katika mwaka 2019/20, serikali imetenga fedha kwa ajili ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaofanyika Oktoba, mwaka huu na maandalizi ya Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwakani 2020,alisema.

Dk Mpango alisema Matumizi ya Maendeleo yanatarajiwa kuwa Sh trilioni 12.248 sawa na asilimia 37.0 ya bajeti yote, kati yake Sh trilioni 9.74 ni Fedha za Ndani na Sh trilioni 2.51 ni Fedha za Nje.

Kati ya Fedha za Maendeleo zilizotengwa, Sh trilioni 2.48 ni kwa ajili ya mradi wa ujenzi wa Reli ya Kisasa (SRG), Sh trilioni 1.44 kwa ajili ya Mradi wa Kufua Umeme Mto Rufiji, Sh bilioni 788.8 kwa ajili ya Mfuko wa Reli, maji na Mradi wa Umeme Vijijini (REA). Shilingi bilioni 450 kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu, shilingi bilioni 288.5 kwa ajili ya ada ya elimu ya msingi.

Aidha, shilingi bilioni 600.0 zimetengwa kwa ajili ya kulipa madeni yaliyohakikiwa ya watumishi, watoa huduma na makandarasi wa barabara, maji na umeme," alisema.

Wabunge wakipitisha bajeti hiyo, wataiwezesha serikali kutekeleza Mipango ya Maendeleo ya nchi hasa mpango wa kila mwaka uliopo ndani ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2016/17- 2020/21), Malengo ya Maendeleo Endelevu 17 (SDGs) ya 2030 na Ilani ya Uchaguzi ya CCM (2015- 2020).

Katika bajeti hiyo maeneo ya vipaumbele ni kuendelea na azma ya kujenga uchumi wa viwanda, kwa kuvutia wawekezaji kwenye viwanda vinavyotumia malighafi zinazopatikana nchini katika mazao ya kilimo, mifugo, uvuvi, misitu na madini, kuzalisha mazao kwa ajili ya soko la ndani na kuuza nje pamoja na kuongeza fursa za ajira.

Inalenga pia kukuza uchumi na maendeleo ya watu, kwa kuimarisha upatikanaji wa huduma bora za afya, elimu na ujuzi, chakula na lishe bora na huduma za maji safi na salama na kuongeza ubora wa nguvukazi ili iendane na mahitaji ya soko la ajira.

Pia uboreshaji wa mazingira wezesha kwa uendeshaji biashara na uwekezaji, kwa kuendeleza ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya reli, bandari, nishati, barabara, madaraja na viwanja vya ndege.

Bajeti inakusudia kuimarisha zaidi ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika ngazi zote. Serikali itaimarisha usimamizi na ukusanyaji wa mapato ya kodi na yasiyo ya kodi ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa bajeti na ukufanyaji wa mapato unafanyika bila kuathiri biashara.

Bajeti hiyo kwa ujumla wake, inalenga kumkomboa Mtanzania na kumtoa katika umasikini kwa kutekeleza sera mbalimbali za mapato na matumizi nchini hasa za kuvutia wawekezaji na ukuaji wa biashara ndogo na za kati.