Naibu Waziri  wa Kazi, Vijana na Ajira, Mhe.  Anthony Mavunde  akizungumza jana na waandishi wa habari pamoja na maofisa wa Bohari ya Dawa (MSD), ambao wapo mkoani humo kwa ziara ya kutembelea wateja wao na kujua changamoto zao.
 Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa Dodoma, Abdul Pumzi, akizungumzia maboresho ya sekta ya afya katika hospitali hiyo. Kushoto ni Mfamasia Mkuu wa jengo la matibabu kwa wagonjwa wa bima ya afya, Betila Haule.
 Muonekano wa jengo la kisasa la wazazi
 Wanafunzi wa udaktari wakiwa mafunzoni ndani ya jengo la wazazi
 Daktari Joab Boaz wa jengo la wazazi akizungumzia upatikanaji wa dawa
 Mfamasia Mkuu wa jengo la matibabu kwa wagonjwa wa bima ya afya, Betila Haule akizungumzia upatikanaji wa dawa.
 Muonekano wa jengo la kisasa la Bima ya Afya
 Afisa Huduma kwa Wateja wa MSD Mkoa wa Dodoma, Inocent Mugisha, akizungumzia jinsi wanavyo sambaza dawa.
Mkazi wa jijini Dodoma, Zakaria Zakaria, akizungumza na waandishi wa habari.

Na Dotto Mwaibale, Dodoma.

UPATIKANAJI wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi vya maabara katika Mkoa wa Dodoma kwa sasa umefikia asilimia 99.8 ukilinganisha na miaka ya nyuma.

Hayo yamebainishwa jana na Naibu Waziri  wa Kazi, Vijana na Ajira, Mhe.  Anthony Mavunde wakati akizungumza na waandishi wa habari pamoja na maofisa wa Bohari ya Dawa (MSD), ambao wapo mkoani humo kwa ziara ya kutembelea wateja wao na kujua changamoto zao.

"Kwa sasa hali ya upatikanaji wa dawa katika mkoa wetu tumefikia asilimia 99.8  tukilinganisha na miaka ya nyuma" alisema Mavunde.

Alisema hali hiyo imetokana na serikali kutenga bajeti kubwa ya fedha katika sekta ya afya na ushirikiano uliopo baina ya viongozi, watendaji wa sekta ya afya pamoja na MSD ambao wanafanya kazi kwa weledi mkubwa.

Mavunde aliipongeza serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Dkt.John Pombe Magufuli kwa kuijali sekta ya afya hasa katika upatikaji wa dawa kila kona ya nchi.

Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa Dodoma, Abdul Pumzi alisema serikali imefanya kazi kubwa kwani hivi sasa hakuna malalamiko ya ukosefu wa dawa katika vituo vya afya na hospitali mkoani humo.

Alisema katika kuboresha huduma za afya kwa wanawake Rais Dkt. John Magufuli alichangia ujenzi wa jengo la kisasa la wazazi huku Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ukitoa mkopo kwa ujenzi wa jengo la kisasa kwa wagonjwa wanaotibiwa kwa bima.

Mfamasia mkuu wa jengo hilo, Betila Haule alisema hivi sasa mauzo ya dawa wanazo pata kutoka MSD baada kujengewa jengo hilo yamepanda kutoka sh.milioni 50 hadi kufikia milioni 500 kwa mwezi.

Afisa Huduma kwa Wateja wa MSD Mkoa wa Dodoma, Inocent Mugisha alisema moja ya mafanikio wanayopata ya usambazaji wa dawa yanatokana na mfumo maalum wa kieletroniki  walio uanzisha wa upatikaji wa taarifa unaojulikana kama “MSD-Customer Portal” unaotumika na wateja wao popote walipo nchini na kuwaondolea usumbufu waliokuwa wakiupata awali wakati wakuagiza dawa, ambapo ili walazimu kusafiri ofisi za Kanda ya MSD inayowahudumia au kupiga simu ili kupata taarifa hizo na nyinginezo.

Mugisha alisema kupitia mfumo huu, MSD imeweza kuongeza ufanisi katika kuhudumia vituo vya kutolea huduma za afya nchini na kuhakikisha adhma ya serikali ya awamu ya tano ya kuboresha huduma za afya kwa wananchi inatimizwa kwa vitendo.

“Mfumo huu umelenga kurahisisha na kuharakisha upatikanaji wa taarifa muhimu zihusuzo dawa, vifaa tiba na vitendanishi vya maabara vinavyotolewa na MSD kwa vituo vya kutolea huduma za afya nchini, kwa kuviwezesha vituo hivyo kupata taarifa muhimu zihusuzo dawa, vifaa tiba na vitendanishi vya maabara kwa wakati popote walipo nchini hata kupitia simu zao za mkononi” alisema, Mugisha.

Aliongeza kuwa mfumo huo, unawawezesha wateja wa MSD kupata taarifa za upatikanaji wa dawa ghalani (stock status) na inakuwarahisi kwao kuagiza mahitaji yao MSD kulingana na matakwa yao kwa wakati husika hata pale wanapokuwa na mahitajiya dharura.

Mkazi wa jijini Dodoma, Zakaria Zakaria ameipongeza Serikali kwa kuboresha upatikaji wa dawa katika Zahanati, Vituo vya afya na Hospitali ukilinganisha na miaka ya nyuma ambapo palikuwa na changamoto kubwa.