Na Stella Kalinga, Simiyu
Mkuu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji nchini Kamishina Jenerali Thobias Andengenye ameliagiza Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, kuendelea kufanya ukaguzi wa kinga na tahadhari ya moto kwa shule zote za sekondari za mabweni nchini kujiridhisha ikiwa vigezo vimezingatiwa, kwa lengo la kuepusha majanga ya moto yanayogharimu maisha ya watu na mali.

Andengenye ametoa maagizo hayo Juni 19, 2019 Mkoani Simiyu wakati akizungumza na wanafunzi wa baadhi ya shule za msingi na sekondari za Mjini Bariadi katika shule ya sekondari Simiyu, katika Halmashauri ya Mji wa Bariadi.

Akizungumza na wanafunzi Kamishina Jenerali Thobias Andengenye amesema kumekuwa na matukio ya moto katika shule kadhaa za bweni ambayo yameleta athari mbalimbali ikiwa ni pamoja na kusababisha vifo kwa wanafunzi, kuteketea kwa mali, hivyo jeshi la zimamoto na uokoaji linaendelea kuweka mikakati ya kukabiliana na majanga hayo. Amesema mikakati hiyo ni pamoja na kusogeza huduma za zimamoto karibu na wananchi kufanya ukaguzi wa tahadhari na kinga ya moto katika majengo, kusoma ramani za majengo na kuanzisha klabu za zimamoto katika shule, ili kuwajengea wanafunzi uwezo wa kujua vitu vya kufanya na vya kuepuka na uwezo wa kukabili moto katika hatua za awali na kuuzima.

Katika hatua nyingine Andengenye amewataka wamiliki wa shule kuzingatia ushauri wa kitaalam unaotolewa na wataalam wakati wa ukaguzi juu ya namna ya kufanya mabweni , madarasa na ofisi ziwe salama kwa kuwasilisha michoro ya majengo hayo katika Ofisi za Zimamoto ili ushauri wa kitaalam uweze kutolewa.

“Niwaombe wanaomiliki shule wazingatie ushauri wa kitaalam unaotolewa, wazingatie ujenzi unaofuata ushauri wa kitaalaam kwa kuwasilisha michoro kama wanataka kujenga mabweni, kuongeza madarasa au kuongeza vyumba vya ofisi basi wazingatie ushauri ili majengo yanayojengwa yawe salama zaidi” alisema.

Aidha, amewaasa wananchi kuacha kuweka mitungi ya gesi ndani na kutikisa mitungi ya gesi kama njia ya kufahamu kiasi cha gesi kilichopo; kwa kuwa kunaweza kusababisha moto na kushauri kuwa njia sahihi ya kupima kiasi cha gesi katika mtungi ni kuweka mtungi katika maji, ambapo baada ya kuutoa sehemu isiyo na gesi itaonekana kuwa kavu.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amesema kumekuwa na mwamko mkubwa wa watu kutumia gesi, hivyo ameshauri Jeshi la Zimamoto na uokoaji kuendelea kutoa elimu katika mikusanyiko ya watu na kupitia vyombo vya habari kuhusu dhana ya matumizi sahihi ya gesi ili kuepusha majanga ya moto.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe. Festo Kiswaga amelishukuru Jeshi la Zimamoto na uokoaji kutoa elimu kwa wanafunzi na akawataka wanafunzi wote waliopata elimu hiyo kuwa mabalozi katika maeneo yao wanayoishi.

Magreth Sonda mwanafunzi wa kidato cha pili shule ya sekondari Simiyu ameshukuru kupata elimu ya tahadhari na kinga dhidi ya moto na kuahidi kuwa yeye pamoja wanafunzi wenzake watakuwa mabalozi wa kueneza elimu hiyo kwa jamii inayowazunguka ili kuepusha majanga ya moto ambayo yana athari nyingi ikiwemo vifo na kuteketea kwa mali.
 Mkuu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji nchini Kamishina Jenerali Thobias Andengenye akiweka kizimia moto katika moja ya vyumba vya madarasa katika shule inayotarajiwa kuwa shule ya wanafunzi wenye vipaji vya michezo Simiyu Sekondari, wakati wa ziara yake Mjini Bariadi Mkoani Simiyu, Juni 19, 2019.
 Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka (kushoto) akimtambulisha Mkuu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji nchini Kamishina Jenerali Thobias Andengenye kwa baadhi ya wanafunzi wa shule za msingi na sekondari za Mjini Bariadi kabla ya kuzungumza nao juu ya kinga na tahadhari ya majanga ya moto wakati wa ziara yake mkoani Simiyu, Juni 19, 2019.
 Mkuu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji nchini Kamishina Jenerali Thobias Andengenye na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka wakiwasha moto kwa ajili ya kuwaonesha wananchi namna ya kuzima moto pindi moto unapotokea, wakati wa ziara yake Mkoani Simiyu, Juni 19, 2019.
 Mkuu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji nchini Kamishina Jenerali Thobias Andengenye akizungumza na wanafunzi wa baadhi ya shule za msingi na sekondari za Mjini Bariadi, kuhusu tahadhari na kinga dhidi ya majanga ya moto,wakati wa ziara yake Mkoani Simiyu Juni 19, 2019.
 Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka(kulia) akimuongoza Mkuu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji nchini Kamishina Jenerali Thobias Andengenye kukagua moja ya mabweni yanayojengwa katika Shule ya Sekondari ya Simiyu, wakati alipotembelea shule hiyo na kuzungumza na wanafunzi wa baadhi ya shule za msingi na sekondari za Mjini Bariadi, kuhusu tahadhari na kinga dhidi ya majanga ya moto,wakati wa ziara yake Mkoani Simiyu Juni 19, 2019.
 Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka(kulia) akimuongoza Mkuu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji nchini Kamishina Jenerali Thobias Andengenye kukagua moja ya mabweni yanayojengwa katika Shule ya Sekondari ya Simiyu, wakati alipotembelea shule hiyo na kuzungumza na wanafunzi wa baadhi ya shule za msingi na sekondari za Mjini Bariadi, kuhusu tahadhari na kinga dhidi ya majanga ya moto,wakati wa ziara yake Mkoani Simiyu Juni 19, 2019.
 Askari wa jeshi la Zimamoto na uokoaji mkoa wa Simiyu, akimuelekeza mmoja wa wanafunzi namna ya kuzima moto wakati wa ziara ya Mkuu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji nchini Kamishina Jenerali Thobias Andengenye katika shule ya Sekondari Simiyu, wakati wa ziara yake Mkoani Simiyu Juni 19, 2019.
Mkuu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji nchini Kamishina Jenerali Thobias Andengenye(katikati) akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa kamati ya Ulinzi naUsalama ya Mkoa wa Simiyu wakati wa ziara yake Mkoani hapa Juni 19, 2019.